• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:50 AM
Sitakuwa dikteta, Ruto aondoa hofu

Sitakuwa dikteta, Ruto aondoa hofu

RAIS William Ruto ameahidi Wakenya kuwa utawala wake hautakuwa wa kidikteta.

Rais Ruto aliyekuwa akizungumza jana katika mahojiano na runinga ya Al Jazeera nchini Amerika alisema kuwa hatafanya maamuzi ya nchi bila kuhusisha idara au viongozi wengine serikalini.

Alisema atakabiliana vikali na maafisa wa serikali watakaokiuka maadili katika serikali yake kwa kutatiza huduma au kujihusisha na ufisadi.

Kiongozi wa nchi alisema baadhi ya watu wanadhani kuwa yeye ni dikteta kutokana na msimamo wake mkali katika utekelezaji wa majukumu yake.

“Mimi nina mazoea ya kushauriana na wengine kabla ya kufanya maamuzi. Watu ambao wamewahi kufanya kazi nami wanakubali kuwa mimi ni muungwana, na hiyo ndiyo maana niliungwa mkono na viongozi wengi katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

“Mimi ni mchapakazi na pia ninahakikisha kuwa malengo yangu yanaafikiwa. Hiyo bidii yangu ndiyo imenifanya kuwa rais. Bila bidii huwezi kufanikisha lolote,” akasema.

Viongozi wa upinzani wamekuwa wakionyesha hofu kuwa huenda Rais Ruto akawa dikteta huku wakimfananisha na marais ambao wameganda mamlakani kama vile Rais Yoweri Museveni wa Uganda ambaye amekuwa kiongozi wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki kwa miaka 35.

Wiki iliyopita Bw Odinga alisema kuwa hatua ya Rais Ruto kufanya kazi kwa karibu na Idara ya Mahakama ilikuwa ishara ya udikteta.

Kadhalika, upinzani umekuwa ukielezea kuwa huenda Rais akabana uhuru wa vyombo vya habari.

Aidha, Rais Ruto alipinga dhana kwamba nchi imegawanyika baada ya uchaguzi huo mkuu.

Kulingana na matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi (IEBC), Rais Ruto alishinda kwa kura milioni 7.8 (asilimia 50.49) huku mshindani wake wa karibu Raila Odinga wa Azimio la Umoja akifuatia kwa kura milioni 6.94 (asilimia 48.85).

“Sidhani kwamba nchi imegawanyika kwa sababu kila upande una majukumu ya kutekeleza. Sisi tutakuwa serikalini na upinzani una jukumu la kuhakikisha kuwa serikali inafanyia Wakenya kazi vyema.

“Serikali ya Kenya itahudumia Wakenya wote bila kujali nani walimpigia kura,” akasema.

Rais alisema kuwa serikali yake itatoa kipaumbele kwa huduma za afya na kukabiliana na umaskini na njaa hasa katika maeno kame.

“Kuna zaidi ya watu milioni 3.1 katika eneo la Kaskazini Mashariki mwa Kenya wanaohitaji chakula kwa dharura. Tunahitaji kufanyia marekebisho bajeti yetu ili tupate fedha za kununua chakula na kuwapelekea msaada waathiriwa wa njaa,” akasema Rais.

Wakati huo huo, Dkt Ruto alisema kuwa serikali yake itaanza wiki ijao mchakato wa kuondoa majina ya Wakenya kwenye orodha ya watu walioshindwa kulipa mikopo (CRB).

“Watu milioni 15 wako ndani ya CRB na hawawezi kuchukua mikopo kwingineko. Tutahakikisha kuwa mfumo mzima wa kuweka watu kwenye CRB unafanyiwa mageuzi,” alisema.

Kulingana na mfumo wa sasa, watu wanaoshindwa kulipa mikopo na kuwekwa CRB, wanazuiliwa kuchukua mikopo kwa kipindi cha miaka mitano.

  • Tags

You can share this post!

Gachagua aahidi kuimarisha usalama eneo la Kerio Valley

Mahakama yatarajiwa kutoa sababu kamili za kutupilia mbali...

T L