• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
Uhuru asema Raila na Mudavadi ndio walimjulisha bungeni

Uhuru asema Raila na Mudavadi ndio walimjulisha bungeni

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta Jumanne alitoa kumbukumbu ya nyakati ambapo alihudumu bungeni kama Mbunge Maalum, Kiongozi wa Upinzani, Waziri na hatimaye Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Fedha.

Akianza hotuba yake ya nane kuhusu Hali ya Taifa, Rais Kenyatta alieleza jinsi alivyojulishwa kwa wabunge na kiongozi wa ODM Raila Odinga pamoja na Kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi.

“Huwa naona fahari kubwa kuwa hapa. Kwanza niliingia bungeni kama Mbunge Maalum ambapo nilijulishwa na Raila Odinga pamoja na Musalia Mudavadi. Baada ya uchaguzi mkuu wa 2022 nilirejea kama kiongozi wa Upinzani na Mbunge wa Gatundu Kusini,” akaeleza.

Rais Kenyatta aliingia bungeni mara ya kwanza alipoteuliwa na Rais wa pili nchini Daniel Moi kuwa mbunge maalum mnamo mwaka wa 2001 baada ya Bw Mark Too kujiondoa.

Baadaye aliwania kiti cha ubunge wa Gatundu Kusini katika uchaguzi mkuu wa 2002 na kumshinda aliyekuwa mbunge, Moses Muhia.

Ni baada ya wakati huo ambapo alipata nafasi ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Serikali za Wilaya na Biashara.

Rais Kenyatta alishinda tena kiti hicho cha Gatundu Kusini katika uchaguzi mkuu wa 2007. Na baada ya kubuniwa kwa serikali ya muungano mkuu chini ya Rais mstaafu Mwai Kibaki na Bw Odinga, Uhuru aliteuliwa kuwa mmoja wa Manaibu wawili wa Waziri Mkuu wakati huo ambapo Waziri Mkuu alikuwa ni Bw Odinga.

Jumanne, Rais Kenyatta akisema kuwa wakati wake bungeni ulimfunza kuwa anaweza kutumikia taifa hili katika wadhifa wowote.

“Huduma ni vitendo sio cheo ambacho mtu anashikilia. Wakati wangu bungeni nilijifunza kuelewa na kufahamu kutangamana na viongozi wa mirengo yote miwili,” akasema Rais Kenyatta.

You can share this post!

Kipusa Alexia Putellas wa Barcelona atawazwa mshindi wa...

Ni Ruto au Raila? PAA yajipata ikijikuna kichwa

T L