• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 5:29 PM
Ushirikiano wa Mudavadi, Ruto waibua tumbojoto huku muungano ukiiva

Ushirikiano wa Mudavadi, Ruto waibua tumbojoto huku muungano ukiiva

Na LEONARD ONYANGO

MUUNGANO wa Naibu wa Rais William Ruto na kiongozi wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi umeendelea kuzua hisia mseto.

Mbunge wa Kanduyi Wafula Wamunyinyi jana Jumatatu alimtaja Bw Mudavadi kama mwanasiasa aliye na tabia ya kuharibia wenzake uwezekano wa kushinda urais.

“Jamii ya Mulembe (Waluhya) imebaini kuwa kila mara uchaguzi wa rais mpya unapokaribia, Bw Mudavadi hujitosa kwenye siasa kuharibia wenzake. Kwa mfano, Bw Mudavadi alijitokeza 2002, 2013 na 2022 kuharibu. Hatuwezi kusaliti jamii kwa kuunga mkono Mudavadi ambaye lengo lake kuu ni kuharibia wenzake,” akadai.

Viongozi wa Kanu na Wiper jana pia walimshambulia Bw Mudavadi huku wakimtaja kama msaliti.

Viongozi wa Kanu waliwataka wakazi wa Magharibi mwa Kenya kupuuzilia mbali muungano kati ya Bw Mudavadi, Dkt Ruto na Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula.

Jumatatu, Naibu wa Rais, Dkt Ruto alisema kuwa tayari wanaandaa mkataba wa maelewano kuhusu namna watakavyogawana nyadhifa ambao watawasilisha kwa Msajili wa Vyama vya Kisiasa.

Hiyo inamaanisha kuwa chama cha Democratic Alliance (UDA) chake Dkt Ruto, Ford Kenya na ANC vitaunda muungano.

Msajili wa Vyama vya Kisiasa, Ann Nderitu jana Jumatatu aliambia Taifa Leo kuwa viongozi hao watatu hawajawasilisha pendekezo la jina la muungano ambao wananuia kutumia. Lakini wandani wa Mudavadi mwaka 2021 waliwasilisha ombi la kumtaka Bi Nderitu kuhifadhi jina la muungano unaofahamika kama Kenya Kwanza.

Jumapili, viongozi kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka na mwenzake wa Kanu Gideon Moi walilazimika kuondoka katika mkutano mkuu wa ANC baada ya kubaini kwamba Dkt Ruto alikuwa miongoni mwa waliofaa kuhudhuria.

“Umesaliti Kalonzo Musyoka na Gideon Moi na huo ndio mwisho wako wa kisiasa,” akasema mbunge wa Mavoko Patrick Makau, Wiper.

Spika wa Bunge Justin Muturi naye alimfokea vikali Bw Mudavadi kwa kuwahadaa vinara wenzake wa muungano wa One Kenya Alliance (OKA) kuhudhuria mkutano wa ANC ambao alitumia kutangaza ushirikiano baina yake na Dkt Ruto.

“Sikuhudhuria mkutano wa ANC lakini nilishangazwa na hatua ya Bw Mudavadi kualika Naibu wa Rais bila kutufahamisha sisi tulioalikwa. Mimi nikiwa kiongozi ambaye alikuwa na uhusiano wa karibu na muungano wa OKA sikuwahi kufahamishwa kuhusu mpango wa kutaka kuungana na Dkt Ruto,” akasema Bw Muturi.

Wandani wa Dkt Ruto, hata hivyo, wanaamini kuwa muungano wa Naibu wa Rais na Bw Mudavadi utawasaidia kuzoa kura kwa wingi katika eneo la Magharibi.

“Hatua ya Bw Mudavadi kuungana na sisi ni ishara kwamba uchaguzi wa urais umeisha na Dkt Ruto anangojea kuapishwa,” akasema Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru.

  • Tags

You can share this post!

MUME KIGONGO: Makapera hatarini kuugua moyo, wanasema...

Mulembe wapongeza Mudavadi, Weta’

T L