• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 5:50 AM
WALIOBOBEA: John Koech: Waziri jasiri aliyekuwa na msimamo thabiti

WALIOBOBEA: John Koech: Waziri jasiri aliyekuwa na msimamo thabiti

KWA HISANI YA KENYA YEAR BOOK

KATIKA eneobunge la Chepalungu, ambako John Kipsang Koech alikuwa mbunge kwa muda mrefu zaidi kati ya 1979 na 2007, wafuasi wake humwita Simba.

Na sio bure.

Alikuwa na msururu wa visa vya uasi vinavyoonekana kuafiki uungwana wake- hii ilimfanya kuwa kama simba na kumtenga na wenzake.

Kwa mfano, mwaka wa 1997, akiwa waziri katika Afisi ya Rais, alienda katika afisi za kampuni ya Nation Media Group mjini Nakuru alipoitisha kalamu na karatasi na kuandika barua ya sentensi moja ya kujiuzulu.

Alikuwa akilalamikia kudharauliwa katika boma la Rais Daniel arap Moi, Kabarak ambako alikuwa amezuiwa kuingia huku wabunge wa kawaida wakiwemo baadhi kutoka wilaya ya Bomet alikotoka wakiruhusiwa kuingia.

Ingawa baadaye Koech alishawishiwa – au kushinikizwa – kubadilisha nia na kurudia kazi yake, alikuwa amejijengea jina kama mmoja wa wanasiasa wenye msimamo katika Kenya, hasa wakati ambao ilikuwa mwiko kukataa uteuzi wa rais na hata kujiuzulu.

Kabla yake ni Mwai Kibaki pekee alikuwa amejiuzulu, miaka sita iliyotangulia.

Kibaki alikuwa Waziri wa Afya wakati huo na alimshangaza Moi siku ya Krismasi mwaka wa 1991 alipotangaza kujiuzulu kupitia kituo cha runinga cha Kenya Television Network kilichokuwa kipya wakati huo.

Tukio la 1997 halikuwa la kwanza la Koech kutofautiana na waliokuwa mamlakani.

Mwaka wa 1989 alifutwa kazi ya waziri wa Ujenzi wa Umma na kutimuliwa kutoka chama cha Kenya African National Union (KANU) – kilichokuwa kilitawala wakati huo- akiwa na Makamu Rais Josephat Karanja kwa “kutokuwa waaminifu” kwa Moi.

Koech aligombea uchaguzi mkuu wa 1992 na akashindwa kwenye uchaguzi mkuu wa 1997, lakini akashinda tena 2002.

Alijiunga na Baraza la Mawaziri hata kama KANU, chama kilichomdhamini bungeni kilikuwa kimeshindwa kwenye uchaguzi.

Waziri huyo wa zamani wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kanda katika serikali ya Kibaki anaamini kwamba alifanya uamuzi uliofaa kwa kujiunga na Baraza la Mawaziri mwaka wa 2004, japo alikuwa mbunge wa upinzani.

Hata kabla ya wakati huo alikuwa amekutana na Kibaki mara nyingi katika miaka mingi waliyohudumu serikalini na kuweza kufanya kazi vyema licha ya kuwa katika vyama tofauti vya kisiasa.

Kwenye mahojiano, Koech alielezea alivyompenda rais huyo wa tatu wa Kenya.

“Kibaki hakutumia pesa visivyo. Katika meza ya Moi, kulikuwa na mkoba uliojaa pesa. Haikuwa hivyo Kibaki akiwa Ikulu,” alisema.

Licha ya kupenda utawala wa Kibaki, mabadiliko ya hali ya siasa wakati huo yalimfanya ahame KANU na kujiunga na chama cha ODM kinachoongozwa na Raila Odinga.

Alipohama Oktoba 11, 2007, alisema kwamba Odinga alikuwa maarufu katika vijiji kote Kenya.

Siku tano baadaye alifutwa kazi ya uwaziri na nafasi aliyoacha ikajazwa na waziri wake msaidizi Wilfred Machage.

Baada ya kushindwa kwenye uchaguzi mkuu wa 2007, na 2013 alipogombea ugavana alistaafu siasa akiwa ameridhika kwamba alikuwa amehudumia vyema wakazi wa eneobunge na nchi.

You can share this post!

Raila aidhinisha Fernandes Barasa awe mrithi wa Oparanya...

SOKOMOKO WIKI HII: Ukachero wa Kabogo ndani ya Kenya Kwanza

T L