• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 5:45 AM
Wanachama KKA wavutania viti serikalini

Wanachama KKA wavutania viti serikalini

NA ONYANGO K’ONYANGO

SIKU chache baada ya Mahakama ya Upeo kuidhinisha ushindi wa Rais mteule William Ruto, mng’ang’anio mkali wa nyadhifa za serikali sasa imeibuka miongoni mwa wandani wake.

Baada ya kuapishwa rasmi mnamo Jumanne, Dkt Ruto atajipata na wakati mgumu kushughulikia masilahi ya wandani wake sasa wanamezea wadhifa za juu katika serikali atakayoiunda.

Taifa Jumapili imethibitisha kuwa mvutano wa sasa ndani ya Kenya Kwanza (KKA) ni kati ya waasisi wa muungano huo na wale waliojiunga nao juzi, haswa kutoka mrengo wa Azimio la Umoja-One Kenya.

Hatua ya Dkt Ruto kushawishi wabunge wa Azimio na wale waliochaguliwa kwa tiketi huru kumsaidia kudhibiti bunge la kitaifa na seneti, hata hivyo haijawafurahisha baadhi ya wandani wake ambao wamesimama naye tangu 2018.

Waanzilishi wa KKA wanadai kuwa wanaojiunga na kambi hiyo baada ya ushindi wa Dkt Ruto wanapania kuvuna mahala ambapo hawakupanda.

Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa anasema hivi: “Licha ya kwamba tunawakaribisha hawa ambao wanajiunga nasi haswa magavana wa zamani, wasitarajie kuteuliwa mawaziri.”

“Viti kama hivyo, vimetengewa wanachama asilia wa Kenya Kwanza wala sio hawa ambao wanajiunga nasi baada ya sisi kupata ushindi,” akaambia Taifa Jumapili jana Jumamosi kwa njia ya simu.

Baada ya Dkt Ruto kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais mnamo Agosti 15, magavana wa zamani Ali Roba (Mandera), Kivutha Kibwana (Makueni) na James Ongwae (Kisii) ni miongoni mwa wanasiasa ambao wamejiunga na kambi ya KKA.

Wengine ni wanasiasa waliopoteza viti vya ugavana na ubunge katika uchuguzi mkuu wa Agosti.

Inatarajiwa kuwa huenda Dkt Ruto akawatunuku wanasiasa hawa nyadhifa kubwa (zikiwemo zile za uwaziri) katika serikali atakayoiunda baada ya kuapishwa Jumanne wiki ijayo.

Lakini tayari wanasiasa wakuu ndani ya KKA, wakiwemo wabunge na maseneta, ni miongoni mwa wale ambao wanamezea mate viti vya uwaziri katika serikali hiyo mpya.

Wao ni wabunge; Aden Duale (Garissa Mjini), Alice Wahome (Kandara) na Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen.

Aidha, duru zilisema kuwa vigogo wengine wa KKA ambao huenda wakatunukiwa nyadhifa za uwaziri ni; aliyekuwa Gavana wa Turkana Josphat Nanok na aliyekuwa Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria.

Hii ina maana kuwa endapo wabunge hao watatu watatunukiwa nyadhifa za uwaziri watajiuzulu na chaguzi ndogo kufanyika katika maeneo bunge yao.

Sababu ni kwamba chini ya Katiba ya sasa wa utawala (urais), wabunge hawateuliwi kutoka bungeni.

Aidha, uchaguzi mwingine mdogo utafanyika katika kaunti ya Bungoma kwa ajili ya kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula.

You can share this post!

DINI: Kunyamaza kwa Mungu si ishara hakupendi

Marais 20 kushuhudia Ruto akiapishwa

T L