• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Wafungwa wadai haki ya ngono na mishahara

Wafungwa wadai haki ya ngono na mishahara

Na WACHIRA MWANGI

Wafungwa katika jela la Shimo la Tewa, Kaunti ya Mombasa wanataka wapewe haki zao za tendo la ndoa na kuongezewa mshahara.

Wafungwa hao pia wanataka wawe wakipewa muda wa kwenda kuwazika wapendwa wao na jamaa wa karibu.

Waliomba Kamati ya Seneti kuhusu Haki na Sheria kuhakikisha kwamba, watakuwa wakienda nyumbani chini ya ulinzi kuomboleza na familia zao.

Kamati hiyo inayosimamiwa na Samson Cherargei ilizuru eneo la Pwani kukagua gereza la Shimo la Tewa Mombasa, na gereza la Kaunti ya Kwale na magereza ya Kaunti ya Kilifi.

Iliambiwa na wafungwa hao kuwa, wanataka serikali iwe ikitunza familia zao wakiendelea kutumikia kifungo chao.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa, haki ya tendo la ndoa imetajwa katika Bibilia na wanastahili kupewa.

Akitoa hoja za wafungwa kwa kamati hiyo, mwakilishi wao Jimmy Obwollah aliomba wafungwa wawakilishwe katika mabunge yote ili kuhakikisha masuala yao yametatuliwa vyema ikiwa ni pamoja na haki ya kupiga kura, na kutaka marekebisho ya sheria za uchaguzi.

“Tutashukuru sana ikiwa serikali itaongeza ufadhili kwa magereza kwa lengo la kununua malazi, vyombo vya kupakuliwa chakula, maji, na bidhaa za kibinafsi kama vile sabuni, karatasi shashi na dawa ya meno kwa sababu wafungwa wengi huwa hawatembelewi na wanahudumu kifungo kirefu,” Bw Obwollah aliambia kamati hiyo.

Wafungwa hao walilalamika pia kuwa, hawana glavu na vifaa vya kujikinga majeraha wakifanya kazi na wakaomba usimamizi wa magereza kuzingatia suala hilo.

Waliomba pia kuchunguza na kubadilishwa kwa mapato ya wanaofanya kazi wakiwa jela.

Bw Obwollah alisema kwa miaka zaidi ya 14 ambayo amekuwa gerezani, mshahara wao ni mdogo sana na hauwezi kufananishwa na bei ya bidhaa wanazotengeneza.

Seneta Cherargei alisema pia kuna haja ya kuchunguza mishahara kuhakikisha kuwa wafungwa wanapoachiliwa wanaweza kuanzisha mradi wa kuwanufaisha.

Alisema tangu uhuru, mishahara ya wafungwa haijawahi kubadilishwa na inashangaza.

“Kwanini tununue bidhaa kwa bei ghali kutoka kwa wafungwa ilhali wanalipwa kitu kidogo?” Hili halifai,” alisema seneta huyo wa Nandi.

You can share this post!

ODM kutolewa pumzi ishara ya kufifia kwa ‘Baba’

TSC kuchunguza vifo vya wanafunzi

adminleo