• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
Madhehebu: Kamati teule kupendekeza Bunge libuni sheria madhubuti

Madhehebu: Kamati teule kupendekeza Bunge libuni sheria madhubuti

NA ALEX KALAMA 

KAMATI teule ya Seneti iliyobuniwa kufanya uchunguzi kuhusu matukio ya maafa ya Shakahola katika Kaunti ya Kilifi, imesema kuwa itapendekeza sheria madhubuti za kudhibiti uhuru wa kuabudu na usalama wa umma.

Inadaiwa kwamba walioangamia walikuwa wafuasi wa mafundisho ya mhubiri tata Paul Mackenzie wa kanisa la Good News International.

Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye ni Seneta wa Tana River Danson Mungatana amesema kuwa kamwe serikali haiwezi kuruhusu tukio kama hilo la maafa makubwa kutokea tena humu nchini kupitia “wahubiri wenye elimu inayokiuka maadili na wanaopotosha waumini.”

Kamati hiyo imezuru chaka hilo la mauti mnamo Jumamosi na ikakumbana na miili ya watu watatu na ambayo ilikuwa imeoza.

Viongozi hao wamekumbana na miili saa chache baada ya kuwasili katika msitu huo.

“Tumezuru eneo ambalo lilipewa jina Galilaya. Huko ndiko Mackenzie aliishi na alikuwa akitoa adhabu na hukumu. Nalo katika eneo lililoitwa Bethlehemu, kamati imeona kulikuwa na kaburi la halaiki ambapo tayari miili 67 ilifukuliwa,” amesema seneta Mungatana.

Aidha mwenyekiti huyo amedokeza kuwa kamati hiyo itahusisha wadau wote katika kushughulikia suala hilo ili kupata muafaka ufaao.

Kwa upande wao baadhi ya maseneta ambao pia ni wanachama wa kamati hiyo wakiongozwa na Tabitha Mutinda wamesisitiza haja ya serikali kukiwezesha kituo cha polisi cha Langobaya ili kuboresha usalama wa eneo hilo.

Naye Seneta wa Migori Eddy Oketch ametoa wito kwa Wizara ya Usalama nchini kuongeza idadi ya maafisa wa usalama wanaoendeleza shughuli ya kuwaokoa manusura katika msitu wa Shakahola.

  • Tags

You can share this post!

Chiloba awatahadharisha Wakenya wasipokee simu kiholela

Arsenal wafika mwisho wa lami

T L