• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Mwanamume ashtakiwa kwa kumuua mzazi sababu ya ‘kumkazia’ pesa za matibabu

Mwanamume ashtakiwa kwa kumuua mzazi sababu ya ‘kumkazia’ pesa za matibabu

NA TITUS OMINDE

MWANAMUME anayedaiwa kumuua babake aliyekuwa na umri wa miaka 68 baada ya mzee huyo kukataa kumpa pesa za kwenda hospitalini kwa matibabu, ameshtakiwa kwa mauaji.

Kijana huyo mwenye umri wa miaka 32 alishtakiwa baada ya ripoti ya uchunguzi wa kimatibabu kutoka hospitalini kuthibitisha kwamba alikuwa sawa kiakili kujibu mashtaka.

Upande wa mashtaka uliamua kumshtaki Silas Mwenda kwa mauaji baada ya ripoti ya pili ya uchunguzi wa akili kutoka Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi (MTRH) mjini Eldoret kuthibitisha kuwa ana akili timamu.

Bw Mwenda, ambaye aliwakilishwa na wakili Damaris Gesare, alikana shtaka la mauaji.

Ripoti ya kwanza ya uchunguzi wa kiakili mwezi mmoja uliopita ilikuwa imeonyesha kuwa hakuwa na akili timamu.

Mahakama ililazimika kuahirisha ombi la kupokea ripoti ya pili ya uchunguzi wa akili.

Ripoti ya pili ya uchunguzi wa kiakili ambayo iliwasilishwa kortini siku ya Ijumaa ilithibitisha kwamba alikuwa timamu kujibu shtaka la mauaji.

Akiwa mbele ya Hakimu Reuben Nyakundi, mahakama iliambiwa kwamba mshtakiwa alimuua babake John Marete mnamo Machi 1, 2023, katika mtaa wa Kipkaren, kaunti ndogo ya Kapseret, Kaunti ya Uasin Gishu.

Katika tukio la siku hiyo, mshtakiwa huyo anadaiwa kuwataka wazazi wake na ndugu zake wengine kumpa pesa ili aende hospitalini kwa matibabu.

Alipokosa kupewa pesa hizo alichukua mashine ya kusaga nyama kutoka kwa nyumba ya babake na kwenda kuiuza ili kupata pesa za matibabu.

Marehemu aliyekuwa na fimbo mbili za mbao alimkabili mwanawe akitaka kujua kwa nini alichukua mashine yake ya kusaga nyama kwa ajili ya kuuza bila ruhusa yake.

Wawili hao walizozana vikali kabla ya mshtakiwa kumzidi nguvu babake na kumpokonya fimbo moja ambayo aliitumia kumpiga mara mbili kichwani.

Mzee huyo alifariki dunia akiwa njiani kupelekwa hospitalini.

Jaji Nyakundi aliagiza kesi hiyo isikilizwe mnamo Desemba 13, 2023.

  • Tags

You can share this post!

Kero kwa Zuchu Tanasha Donna akimpa Mama Dangote zawadi ya...

Antony anayekabiliwa na tuhuma za kuwadhulumu wanawake...

T L