• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 1:22 PM
Machifu maadui wa maendeleo wamulikwa Kilifi

Machifu maadui wa maendeleo wamulikwa Kilifi

NA MAUREEN ONGALA

WAKAZI wa eneobunge la Ganze wamewanyooshea kidole cha lawama machifu katika eneo hilo kwa kuwa kikwazo katika juhudi za jamii kujua haki zao katika maswala ya maendeleo.

Walieleza kuwa mara nyingi machifu wamepinga vikali vikao vya jamii vinavyoandaliwa na wakazi hao kuhusu maswala ya uongozi na maendeleo.

Wakizungumza katika kikao maalum kilichoandaliwa na shirika la kijamii la Kenya Community Support Centre [KECOSCE] katika wadi ya Ganze kuhamasisha jamii kuhusu sheria ya ushiriki wa umma ya Kilifi County Public Participation and Civic Education Act, 2020, viongozi hao wameeleza kuwa imekuwa changamoto kuwafikia wanajamii kwa sababu ya vikwazo kutoka kwa machifu.

Walisema licha ya kuwa wamepewa uwezo wa kuzunguka katika jamii na kuwaelimisha kuhusu haki zao, machifu wameonyesha kutoridhishwa na hatua hiyo na hutaka kuwanyamazisha.

Katibu wa kikundi cha walemavu cha Lemalema kutoka wadi ya Bamba Bw Daniel Nyongo alisema kuwa mara mingi machifu pia wamekosa kuwahusisha jamii katika mikutano yao ya kujadili maswala ya jamii.

“Mara kwa mara machifu wanafanya mikutano ambayo inahudhuriwa na baadi ya watu wachache waliochaguliwa na kuna mambo muhimu ambayo yalichipuka yalijadiliwa. Kinachotusikitisha ni kuwa jamii inajua kuhusu mikutano hiyo baada ya hata siku tano,” akasema Bw Nyongo.

Bw Nyongo alisema kuwa hata baada ya mmoja wa machifu aliyehudhuria kikao hicho kukiri kuwa wanastahili kuandaa vikao visivyopungua 10 kila mwezi, bado wananchi wanazidi kutengwa.

Alisema kuwa hali hii imechangia changamoto kubwa kuhusu jinsi jamii inavyohusiswa na kuchangia au kutoa mapendekezo yao katika mikutano kama hiyo.

“Kuna sehemu nyingine ambapo tumekatazwa kabisa kufanya mikutano licha ya sisi kutangaza nia yetu ya kuandaa vikao hivyo vya hamasa kupitia afisi za naibu msaidizi wa kamishna na machifu,’’ akasema.

Bw Ngonyo alisema kuwa machifu hupiga simu na kudai kuwa hawana ufahamu na mikutano hiyo.

“La kushangaza ni kuwa machifu hao huwa na habari kuhusu mikutano hiyo ya hamasa ambayo imeidhinishwa na wakubwa wao,” akasema.

Alisema tabia ya machifu hao inadhihirisha kwamba kuna mambo fiche katika jamii ambayo hawataki yajulikane.

Bw Ngonyo alitoa mfano wa masaibu aliyokumbana nayo siku moja alipokuwa ameandaa kikako katika eneo la Shirango katika kata ndogo ya Gede.

“Nilikuwa na kikao katika afisi ya naibu wa chifu mmoja na nikabiiwa simu na mwenzake ambaye alikuwa katika pilkapilka zake kunitaka nisitishe mkutano huo mara moja. Muda mchache akampigia yule naibu wa chifu huku akimzomea na pindi tu alivyokata simu, nikaamurishwa kutoendelea na mkutano huo,” akasema.

Alisema wakati umefika machifu wawajibike na kukoma kuwazuia jamii kujadili maswala yanayowausu.

“Tunataka machifu wawajibike katika utendaji kazi wao kwa sababu akuna jambao linalohusu mwananchi ambalo aliwezi jadiliwa popote,” akasema.

Alitoa wito kwa viongozi kushirikiana na wakazi kwa minajili ya maendeleo na manufaa ya jamii.

Kila mara wakazi katika eneobunge hilo wamewanyooshea machifu katika eneo hilo kidole cha lawama kwa kufanya mambo kinyume na mapenzi yao na hata pia kuwakandamiza.

Machifu hao wamelaumiwa pakubwa kuchangia mizozo baina ya jamii ya wafuaji na wenyeji kwani wao husimamia mikataba mingi ya mashamba wakati wenyeji wanapowakodishia wafugaji sehemu za malisho.

Wakazi hao wamekuwa wakilalamika ya kwamba wakati mwingi wafugaji hukiuka mikataba hiyo na kuanza kuwadhulumu wenyeji huku machifu wakiwaunga mkono.

Pia, machifu wamelaumiwa pakubwa kwa kubagua wakazi wakati wa shughuli ya kugawa chakula cha msaada hali ambayo imechangia wengi wao kuendelea kutaabika na makali ya njaa.

Afisa msimamizi wa mipango katika shirika la KECOSCE Bw Maxwel Lumbasi alisema kuwa viongozi wa masinani wamekuwa wakiwa tena wanajamii kwenye maswala ya maendeleo na pia kupaza sauti ya mambo yanayowahusu.

“Katiba ya Kenya inampa mwananchi nafasi ya kuchagua ni nini anachotaka itendeke na kuwapa vionozi uwezo wa kutulindia na kutupangia raslimali yetu,’’akasema.

Alisema kuwa sharia hiyo ni muhimu kwani inatoa mwongozo jinsi wananchi wataketi pamoja na vionozi wao katika mipanilio ya maswala ya maendeleo.

Sheria hiyo pia inatoa mwongozo jinsi wananchi watapata habari juu ya miradi katika sehemu zao kupitia kamati ndogondogo ambazo zimeundwa na jinsi watakavyofatilia na pia uwajibikaji wa viongozi na wananchi katika maswala ya maendeleo.

Shirika hilo limewaleta pamoja mashirika 163 ya kijamii katika Kaunti ya Kilifi yanajiusisa na maswala ya uongozi na kuwapa mafunzo na uwezo kuakikisa seria hii inatekelezwa vilivyo.

Bw Lumbasi alisema kuwa wanatajaria kuwapa mafunzo kamati zote ndogo za maendeleo mashinani kufikia mwisho mwezi wa saba.

Afisa anayesimamia maswala ya elimu kwa jamii katika Kaunti ya Kilifi Bw George Deche alisema kuwa ipo haja ya mashirika kujitokeza na kuwapa wanajamii elimu ya kutosha kuhusu sheria hiyo.

Kwa sasa Kaunti ya Kilifi inaendelea na mikakati ya kubuni sera itakayotoa mwelekeo wa jinsi ya kutekeleza sheria hiyo kwa ukamilifu.

Alitoa wito kwa wakazi wa Kilifi kuwajibika na kuhakikisha kuwa sheria hiyo inatekelezwa kwani inawahusu moja kwa moja.

“Mara nyingii wananchi wetu wamekuwa wakiangalia maswala ya maendeleo kama watazamaji tu, lakini ni wakati wa kuwa mstari wa mbele katika utekelezaji wa sheria hii ili wapate faida kamili kwa maswala yote yanayousu utendakazi wa serikali,’’ akasema Bw Deche.

Mwanachama wa kundi la kijamii la Bareko kutoka wadi ya Bamba Bw Gideon Charo alisema kuwa mara mingi machifu hao wamewaita wapinzani wa serikali.

“Tunapata pingamizi wakati wa kuwahamasisha wananchi kuhusu haki zao, na pia mambo ya miradi na maendeleo kutoka kwa serikali kuu na ya kaunti na kila mara machifu husema sisi ni wapinzani wa serikali,’’ akasema.

Alisema hali hiyo inalemaza juhudi za viongozi wa kijamii kutetea haki za wananchi mashinani.

Bw Lawrence Mbuko kutoka wadi ya Sokoke alisema kuwa itakuwa bora ikiwa viongozi wa serikali ya Kaunti ya Kilifi na serikali ya kitaifa watahakikisha ya kuwa mwananchi anafurahia ugatuzi akiwa mashinani.

“Ni lazima viongozi wetu wahakikishe kuwa mwananchi anajua jukumu lake na anahusishwa vilivyo katika kila swala la maendeleo kupitia ngazi husika,” akasema Bw Mbuko.

 

  • Tags

You can share this post!

Shule moja nchini Nigeria yawaruhusu wazazi kulipa karo kwa...

Infinix yazindua simu mpya aina ya NOTE 30 series

T L