• Nairobi
  • Last Updated October 2nd, 2023 10:18 AM
Shule moja nchini Nigeria yawaruhusu wazazi kulipa karo kwa taka

Shule moja nchini Nigeria yawaruhusu wazazi kulipa karo kwa taka

NA MASHIRIKA

LAGOS, Nigeria

SHULE moja viungani mwa jiji la Lagos nchini Nigeria imewashangaza wengi kwa kubuni njia ya kipekee ya kusuluhisha shida ya ukosefu wa karo inayowasibu wanafunzi wake.

Shule hiyo ya My Dream Stead School iliyoko katika kitongoji cha Ajegunle inakubali aina mbalimbali za taka kama karo. Shule hiyo ni mojawapo ya shule 40 za karo ya chini viungani wa Lagos.

Mwanafunzi Fawas Adeosun ni mmoja wa wanafunzi kutoka familia za kipato cha chini ambaye amefaidi kutokana na mpango huo baada ya mamake, Fatimoh, kuruhusiwa kumlipia karo kwa njia hiyo.

Kwa miaka minne iliyopita, shirika moja la kimazingira kwa jina African Cleanup Initiative limekuwa likikusanya chupa, mikebe, na chupa za plastiki zinazoletwa katika shule hiyo ya My Dream Stead na wazazi na kuziuza kwa kampuni za kutengeneza bidhaa za matumizi kutokana na takataka.

Pesa zinazopatikana kutokana na mauzo ya taka hizo zinatumika kulipa mishahara ya walimu, kununua sare za wanafunzi, vitabu na kalamu miongoni mwa mahitaji mengine.

Mpango huo unalenga kupunguza idadi ya watoto wasioenda shuleni sambamba na kupunguza mrundiko wa taka katika barabara za Lagos, akasema Alexander Akhigbe, mwanzilishi wa kundi hilo la uhifadhi wa mazingira.

Karo ya masomo katika shule ya My Dream Stead ni dola za Amerika 130 (Sh18,800) kwa mwaka. Shule hiyo inaendelea kupanuka baada ya kukamilishwa kwa jengo lingine ambalo litasitiri wanafunzi 120.

Shule huyo ilianzishwa mnamo mwaka wa 2019 kwa watoto saba pekee.

Nyakati za asubuhi, Mama Fatimoh na mwanawe Fawas kwa pamoja hubeba magunia ya taka mabegani mwao kuelekea shuleni humo.

Taka hizo hupimwa uzani na mauzo yake hujumuishwa kwenye akaunti ya karo ya Fawas.

“Nyakati fulani akitaka kununua vazi la michezo, shule itanijulisha kuhusu kiasi cha taka cha kuleta ili kitosheleze ununuzi wa vazi hilo,” akasema Fatimoh ambaye ni msusi mwenye umri wa miaka 48. Yeye ndiye hugharimia malezi ya wanawe kivyake.

Tafsiri: CHARLES WASONGA

  • Tags

You can share this post!

Mackenzie aambia Kindiki anachopigana nacho kitamramba

Machifu maadui wa maendeleo wamulikwa Kilifi

T L