• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 7:55 PM
Magavana wa Pwani wapata presha kali kuungana

Magavana wa Pwani wapata presha kali kuungana

ALEX KALAMA na VALENTINE OBARA

SHINIKIZO imezidi kutolewa kwa magavana watatu wa Pwani waepuke kutengana katika uchaguzi ujao.

Magavana Salim Mvurya (Kwale), Hassan Joho (Mombasa) na Amason Kingi (Kilifi) wamechukua mielekeo tofauti kuhusu uchaguzi ujao, hasa wa urais watakapokamilisha vipindi vyao vya pili vya uchaguzi.

Bw Mvurya anaegemea upande wa Naibu Rais William Ruto, huku Bw Joho akiunga mkono azimio la Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga.

Kwa upande wake, Bw Kingi ameashiria atamuunga mkono Bw Odinga kwa urais ingawa amesema atapigia debe wanasiasa watakaowania viti vingine kupitia Chama cha Pamoja African Alliance (PAA).

Misimamo hii mikali imesababisha baadhi ya viongozi wa kijamii na wanasiasa kuonya kuwa Pwani itakuwa hatarini kukosa nafasi nzuri katika meza ya serikali ya kitaifa baada ya uchaguzi ujao.

Kulingana na wadadisi wa kisiasa, hii ni kutokana na kuwa maeneo hupata ushawishi ndani ya serikali kwa msingi wa idadi ya kura ambazo eneo hilo lilitia kwenye kapu la kura za urais.

Wazee wa jamii za Wamijikenda sasa wamesisitiza kuwa ni sharti watatu hao wazike tofauti zao kwa minajili ya kuwatumikia Wapwani.

Wakiongozwa na Katibu Mkuu wa muungano wa kitamaduni wa kaya za Wamijikenda Malindi, Bw Joseph Karisa Mwarandu wazee hao walisema Pwani haitapata sauti moja kisiasa 2022 ikiwa watatu hao watakuwa bado wametengana.

“Tunataka hawa viongozi wa Pwani waeke ubinafsi kando na waangalie yale matatizo ambayo yanawakabili watu wa Pwani na waangalie ni jinsi gani wataweza kuyatatua. Huku kuendelea kutofautiana hakusaidii Wapwani bali kunazidi kuwafanya wateseke zaidi,” akasema Bw Mwarandu.

Kulingana na wazee hao, matatizo ya Wapwani ikiwemo masuala ya umiliki wa ardhi, yatapata suluhu la kudumu endapo viongozi hao watasimama na kuzungumza kwa kauli moja.

“Hizi shida ambazo zinaikumba jamii ya Pwani hasa likiwemo suala tata la ardhi zinaweza kutatuliwa endapo viongozi wetu wataeka tofauti zao kando na kushirikiana katika kutafuta suluhu ya mambo haya,” alisema Bw Mwarandu.

Wanasiasa wa Pwani ambao huwataka watatu hao waungane, huwa wanatofautiana kuhusu upande ambao wanafaa kuegemea katika uchaguzi ujao wa urais.

Wamegawanyika pande za ODM, United Democratic Alliance (UDA), na Pamoja African Alliance (PAA) ambayo inaongozwa na Bw Kingi.

Wakati wa mkutano wa Azimio la Umoja mjini Nairobi ambapo Bw Odinga alitangaza rasmi atawania urais, Bw Joho alisisitiza kuwa waziri mkuu huyo wa zamani ndiye ana uwezo wa kutatua changamoto nyingi zinazokumba taifa hili.

Miongoni mwa wanasiasa ambao humshinikiza Bw Joho ajiunge na UDA ni Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, ambaye hudai kuwa Pwani haijanufaika katika miaka yote ambapo ilikuwa ikifuata ODM.

“Kutakuja wakati ambapo nitasimulia mambo mazito ambayo Baba (Bw Odinga) hawezi kuwaambia. Wakati utafika tutafichua yote. Wale ambao wanasema tuachane na historia, nawaambia hutaelewa ya usoni usipojua yaliyopita,” akasema Bw Joho.

Kwa upande wake, licha ya Bw Kingi kuashiria kuwa ataegemea upande wa Bw Odinga kwa urais, inasubiriwa kuonekana ikiwa ODM itakubali kushirikiana naye kwa msingi wa uamuzi wake kuwa PAA itasimamisha wagombeaji wa viti vingine vyote vya kisiasa.

Gavana huyo alisisitiza wiki iliyopita kuwa, uamuzi wake kuunda PAA ni kwa minajili ya kuwapa Wapwani chama ambacho wanaweza kutumia.

You can share this post!

Wagombeaji ugavana Homa Bay wakimbilia koo kujitafutia...

TAHARIRI: CBC: Serikali ijitahidi kutoa mwelekeo faafu...

T L