• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 3:55 PM
Azimio wamtaka Rigathi akae kando ya mazungumzo

Azimio wamtaka Rigathi akae kando ya mazungumzo

NA WINNIE ATIENO

WANASIASA wa mrengo wa Azimio la Umoja One Kenya kutoka Mombasa, wamemtaka Naibu Rais, Bw Rigathi Gachagua, asijihusishe na mazungumzo ya upatanisho wa muungano huo na Kenya Kwanza.

Wakiongozwa na wabunge Mishi Mboko (Likoni), Omar Mwinyi (Changamwe) na Mbunge Mwakilishi wa Kike katika Kaunti ya Mombasa, Bi Zamzam Mohamed, walisema mazungumzo hayo hayamhusu Bw Gachagua bali ni ya Rais William Ruto na kinara wao, Bw Raila Odinga.

“Kazi ya Bw Gachagua ni kuharibu kila anakoenda. Sisi tunamwambia kaa kando. Wale waliopigiwa kura ni watu wawili, Bw Ruto na Bw Odinga, wewe kaa kando, wazungumze tujue hatima yetu,” akasema Bi Mohammed Wanasiasa hao pia wamewakashifu wenzao wa Kenya Kwanza kwa kuhujumu mazungumzo ya mapatanisho kati ya Rais Ruto na Bw Odinga.

Walisema wenzao wa Kenya Kwanza hawana nia ya kufanikisha mazungumzo ya mapatanisho.Wakiongea kwenye hafla ya kupeana hundi ya Sh16 milioni kwa makundi ya wanawake wa Mombasa eneo la Bomu, viongozi hao waliwataka wanasiasa wa Kenya Kwanza kumheshimu Bw Odinga.

Walimkosoa Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Taifa, Bw Kimani Ichung’wa, na Mbunge wa Kiharu, Bw Ndindi Nyoro, kwa matamshi wanayosema ni ya kumdharau Bw Odinga.

“Tunaomba watu wa Kenya Kwanza wawe na subira na heshima kwenye haya mazungumzo,” akasema Bw Mwinyi.Alisema mazungumzo hayo yanafaa kusimamiwa na watu wenye busara katika mrengo wa Kenya Kwanza kwani kulingana naye, wale waliochaguliwa wameonyesha hawana nia ya kutafuta upatanishi.

“Wanaongea upuzi, maneno yao yanachafua roho za asilimia 50 za wapigakura nchini Kenya,” akasema.

Bw Mwinyi aliongeza kuwa, wanasiasa ambao wana misimamo mikali na kumtishia Bw Odinga kuhusu nia ya kurudi kwenye maandamano wana nia mbaya.

“Tukitaka maandamano tutarudi barabarani. Hatutakata tamaa wala kuogopa,” aliongeza.

Kwa upande wake, Bi Mohamed alisema Bw Odinga anafaa kuheshimiwa na wanasiasa wote.

“Bw Ichung’wa na mwenzake Nyoro wanafaa kumheshimu Bw Odinga ambaye amepigania taifa hili. Tunataka Kenya isonge mbele, lakini kuna wanasiasa wa Kenya Kwanza ambao wamekuwa wakimtukana Bw Odinga tukiwaangalia tu, sisi wanajeshi wake tuko macho,” akasema Bi Mohammed.

Masuala kuhusu mazungumzo hayo yanayotarajiwa kuanza wiki hii yalipewa uzito katika ziara ya Rais Ruto eneo la Kati.Ziara hiyo iliyodaiwa kuwa na kuzindua miradi ya maendeleo iliishia kuonekana kama ulingo wa kuwashawishi wakazi wa Mlima Kenya kwamba viongozi wa upinzani hawatashirikishwa ndani ya serikali waliyochagua kwa wingi kuingia mamlakani.

Awali alipozuru Pwani, suala hilo pia lilijadiliwa kwa upana katika mikutano yake na viongozi ambapo wengi walipuuzilia mbali mazungumzo kati ya upinzani na serikali.

Hata hivyo, Bw Odinga ameeleza wazi kwamba hana haja ya kuingia serikalini huku akipuuzilia mbali madai kwamba alitumia handisheki kuingia katika serikali ya aliyekuwa rais Uhuru Kenyatta, na Dkt Ruto aliyekuwa naibu wake.

Viongozi hao walisema wako tayari kurudi kwa maandamano endapo Kenya Kwanza itakataa kutimiza matakwa ya Bw Odinga.Vilevile, walimtaka Bw Ruto kukabiliana na ufisadi serikalini.

 

  • Tags

You can share this post!

Lawrence Munga: Pesa kwangu si hoja, hutumia zaidi ya Sh40,...

Polisi wapata afueni kwenye kesi ya mauaji

T L