• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 10:50 AM
Maadhimisho Jamhuri Dei 2021: Rais Kenyatta asifia Raila Odinga

Maadhimisho Jamhuri Dei 2021: Rais Kenyatta asifia Raila Odinga

Na SAMMY WAWERU

SHEREHE za madhimisho ya Jamhuri Dei 2021 zimefanyika Jumapili, katika Bustani ya Uhuru, jijini Nairobi.

Rais Uhuru Kenyatta ameliongoza taifa katika maadhimisho hayo ya Makala ya 58, yanayosherehekewa kila mwaka, baada ya Kenya kuwa Jamhuri Desemba 12, 1963. Kati ya viongozi wenye nyadhifa kuu serikalini na wanasiasa waliohudhuria, ni naibu wa rais, Dkt William Ruto, kinara wa ODM, Raila Odinga na mawaziri.

Kwenye hotuba yake, kiongozi wa nchi alitumia jukwaa hilo kummiminia sifa chungu nzima Bw Raila, kwa kila alitaja “kuwa mshauri wangu mkuu wa maendeleo”. Akimshukuru, Rais Kenyatta alisema kiongozi huyo wa upinzani alimpa wazo la kuimarisha Uhuru Gardens.

“Ningetaka kumtambua mmoja wetu katika maadhimisho haya, na ambaye amenifaa kwa dhati, ndugu yangu Raila Odinga. Alinipa ushauri kuboresha bustani hii ambayo imetumika kuadhimisha Makala ya 58 ya Jamhuri Dei,” Rais akaelezea.

Kwa upande wake Bw Raila, alisema endapo si jitihada za upesi za Rais ardhi ya bustani ilikuwa katika harakati za kunyakuliwa. “Ninakushuru sana ndugu yao, Uhuru Kenyatta kwa kuokoa Uhuru Gardens kutoka mikononi mwa wanyakuzi wa ardhi na mashamba,” akasma.

Wawili hao wamekuwa wakishirikiana kwa karibu, hasa baada ya maridhiano kati yao, mnamo Machi 2018. Licha ya naibu rais Ruto kudai Handisheki imesambaratisha mikakati ya serikali tawala ya Jubilee, Rais na Waziri huyo Mkuu wa zamani wanasifia ushirika wao wakihoji umechangia kudumisha amani nchini.

Dkt Ruto analalamikia mahesabu yake kumrithi Rais Kenyatta kusambaratishwa na Handisheki. Aidha, Rais amenukuliwa mara kadha akisema amefanya maendeleo kibao baada ya wawili hao kutangaza kuzika tofauti zao, ikilinganishwa na awamu ya kwanza, 2013 – 2017.

Rais Kenyatta vilevile amekuwa akisisitiza kwamba atakapostaafu mwaka ujao, hatakubali kuachia serikali viongozi anaotaja kuwa ni “mafisadi na wafujaji wa mali umma”. Siku mbili zilizopita, Bw Raila alitangaza kwamba atawania urais 2022, na ambapo amepata uungwaji mkono na muungano wa wafanyabiashara kutoka Mlima Kenya (MKF), katika safari yake kuingia Ikulu.

MKF inajumuisha mabwanyenye wenye ushawishi mkuu nchini katika sekta ya biashara na uchumi.

You can share this post!

Uhuru aapa kuwa BBI itatimia

Mizomo ya wafuasi wa Maina Njenga kwa Ruto yachemsha kambi...

T L