• Nairobi
  • Last Updated June 12th, 2024 4:24 PM
Mama mkwe wa Maina Njenga azirai akilishwa kiapo kortini

Mama mkwe wa Maina Njenga azirai akilishwa kiapo kortini

Na JOSEPH OPENDA

Kesi ya Kiongozi katika muungano wa Azimio Maina Njenga kuhusiana na ushiriki wake kwenye kundi haramu la Mungiki na maovu yaliyotendeka katika eneo la Bahati, Nakuru ilianza kwa hali ya ati-ati Jumatatu, Novemba 20, 2023.

Bw Njenga ambaye hufahamika zaidi kama kiongozi wa zamani wa kundi la Mungiki aliwekwa kujibu mashtaka baada ya jaribio lake kusitisha kesi hiyo ambapo yeye pamoja na wengine 11 wanakabiliwa na mashtaka saba liligonga mwamba.

Hakimu Mkuu wa Nakuru Kipkurui Kibellion alitupilia mbali ombi lililokuwa limewasilishwa na kikosi cha mawakili cha Bw Njenga, kikiongozwa na Steve Biko, ambaye alishutumu serikali kwa kugeuza baadhi ya washukiwa kuwa mashahidi bila kufuata sheria.

“Baadhi ya ripoti za mashahidi ambazo tumepewa zilirekodiwa na washukiwa,” akasema Bw Biko.

“Uamuzi wa upande wa mashtaka kugeuza washtakiwa kuwa mashahidi dhidi ya Bw Njenga haukufanywa ifaavyo kwa sababu hakukuwa na ombi kama hilo lililowasilishwa kortini likitaka hatua kama hiyo.”

Bw Njenga vilevile alitaka kesi hiyo isitishwe akisema ilifanana na nyingine anayokabiliana nayo katika mahakama ya Makadara, Nairobi.

Hakimu alitupilia mbali ombi lake, akisema alishindwa kuwasilisha ushahidi kuelezea pingamizi zake hivyo basi akazipata hazina mashiko.

Bw Njenga na washtakiwa wenzake wanakabiliwa na mashtaka saba yanayohusiana na ushirika na kundi lililoharamishwa la Mungiki, kushiriki katika uhalifu eneo la Bahati kati ya Mei 11 na 18, 2023.

Kulizuka kizaazaa kesi ilipokuwa inaanza, wakati shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka, ambaye ni mama mkwe wa Bw Njenga, alipozirai akipewa kiapo kabla ya kuanza kuulizwa maswali.

Shahidi huyo ambaye ni mama mkongwe aliyetambuliwa kama Hannah, alizirai na kuanguka muda mfupi baada ya kupandishwa kizimbani kutoa ushahidi dhidi ya mkaza mwana wake na kufanya wahudumu wa mahakama kukimbia kumsaidia.

Chanzo cha kuzimia kwake hakikutambuliwa mara moja.

  • Tags

You can share this post!

Mambo yamechemka: Mulamwah, Ruth K watangaza wanatarajia...

Msaada hatimaye wawasili Lamu kunusuru wakazi wanaozongwa...

T L