• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Msaada kwa walioathirika na mafuriko Nakuru

Msaada kwa walioathirika na mafuriko Nakuru

Na MERCY KOSKEI

ZAIDI ya familia 50 kutoka wadi ya Soin na Murindat, Kaunti ya Nakuru zilizoathirika na mafuriko kutokana na mvua inayoendelea zimenufaika na chakula kutoka kwa Gavana Susan Kihika.

Familia hizo zilipokea msaada huo kutoka kwa serikali ya Kaunti kupitia kwa idara ya kukabiliana na majanga, ilipotembelea waathiriwa hao.

Katika Kijiji cha Lomolo, Soin nyumba zaidi ya 15 zilisombwa na maji na mali ya thamani isiyojulikana kuharibiwa.

Hata hivyo, hakuna kisa chochote cha maafa kutokana na mafuriko kiliripotiwa.

Wakazi wadi ya Soin na Murindat, Kaunti ya Nakuru wakipokea chakula cha msaada kufuatia athari za mafuriko. Picha / MERCY KOSKEI

Akizungumza baada ya kupeana msaada huo, Bw John Macharia aliyemwakilisha Afisa Mkuu wa Kukabiliana na Maafa, Bi Joyce Ncece, alisema kaunti itatafuta njia mbadala kusaidia walioathirika.

Familia hizo zilipokea mahindi, maharagwe, mtama, mchele na ndengu, huku wakiomba usaidizi zaidi wa vifaa vya kujenga upya nyumba zao zilizosombwa na maji na pia malazi.

Kwa upande wake, diwani eneo hilo, MCA, Naburuki Degaulle aliwasihi wakazi hao kuhama kutoka maeneo yanayochukuliwa kuwa njia asili ya maji ili kujiepusha na majanga kama hayo siku zijazo.

Baadhi ya kina mama waliopata chakula cha msaada, wanaomba wahisani na wasamaria wema kuwasaidia malazi. Picha / MERCY KOSKEI

Naburuki ambaye pia ni mwenyekiti kamati ya kukabiliana na maafa katika Bunge la Kaunti, alizidi kuwasihi wakazi hao kutoishi katika maeneo yanayojulikana kuwa hatari kwa mafuriko.

Maoni yake yaliungwa mkono na naibu chifu kata ya Lomolo Bw Korkoren Leonard, ambaye alisisitiza umuhimu wa kuondoka kutoka kwa maeneo yanayokumbwa na mafuriko akisema kuwa maisha ya watu yamo hatarini.

Mojawapo ya nyumba zilizosombwa na mafuriko. Picha / MERCY KOSKEI

Familia zingine tatu kutoka Ebburu Mbaruk, Nderit Elementaita ambazo pia ziliathirika na mafuriko kutokana na mvua kubwa iliyonyesha Alhamisi usiku zilipokea chakula cha msaada.

Bw Joseph Soi mkaazi wa Soin alisema kuwa walioathirika wanaishi kwa majirani huku wakisubiri kusaidiwa kujengewa nyumba kabla ya kurudi walikokuwa wanaishi.

“Tunafurahi kwa msaada ambao tumepata hii leo, ila tungeomba mtusaidie zaidi kwani hata sasa hatuna pa kulala.

“Tunamshukuru Mungu hakuna aliyepoteza maisha, ni majeraha tu,” alisema David Laboso mkazi mwingine.

  • Tags

You can share this post!

Uhuru alivyozamisha merikebu ya Jubilee

Zubeidah Kananu achaguliwa kuwa rais wa Baraza la Wahariri...

T L