• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 6:55 AM
Rais Kenyatta ahutubia taifa kupitia kikao cha pamoja bungeni

Rais Kenyatta ahutubia taifa kupitia kikao cha pamoja bungeni

Na SAMMY WAWERU

RAIS Uhuru Kenyatta anahutubia taifa leo Jumanne alasiri katika kikao cha pamoja cha bunge, wengi wakisubiri kusikia mipango ya serikali kusaidia kuokoa uchumi kufuatia athari za janga la Covid-19.

Kabla kulakiwa bungeni na maspika, Bw Ken Lusaka (seneti) na Bw Justin Muturi (kitaifa) na kuanza kutoa hotuba, kiongozi wa nchi alikagua gwaride la heshima, lililoandaliwa nje ya makao ya bunge na kikosi cha majeshi Kenya (KDF).

Kenya ilikumbwa na virusi vya corona mapema 2020, janga la kimataifa ambalo limeathiri uchumi na sekta mbalimbali.

Baadhi ya biashara zimefungwa, mamia na maelfu ya watu wakipoteza nafasi za ajira kipindi ambacho gharama ya maisha inazidi kupanda.

Bei ya bidhaa za kula, hasa unga, sukari, mafuta ya kupika, mchele, kati ya zinginezo inaendelea kuwa ghali.

Mafuta ya petroli aidha yanazidi kuwa ghali, hatua ambayo imechangia mfumko wa bei za bidhaa zinazohusisha mwananchi wa kawaida, na katika hotuba ya Rais Kenyatta kwa taifa wanachi wana hamu kuskia iwapo atapunguza ushuru (VAT).

Huku hotuba ya Rais ikijiri wakati ambapo taifa na ulimwengu lina wasiwasi kuhusu mchipuko wa aina mpya na hatari ya corona kutoka Afrika Kusini, haijulikani ikiwa atatangaza kukaza kamba sheria na mikakati ya Wizara ya Afya (MoH) kusaidia kuzuia msambao.

“Bado tungali katika hatari, Covid-19 haijaisha,” amesema Rais Kenyatta, akielezea hatua ambazo serikali imepiga katika kupambana na virusi vya corona.

Hata ingawa kirusi hicho, Omicron, hakijaripotiwa hapa nchini, Shirika la Afya Duniani – WHO limeonya kuwa kinasambaa kwa kasi.

Chanjo ya corona inaendelea kutolewa, wananchi wakihimizwa kujitokeza kudungwa sindano ili kuzuia makali ya homa hiyo hatari.

Naibu wa Rais, Dkt William Ruto, kiongozi wa ODM, Raila Odinga, Musalia Mudavadi (ANC), Kalonzo Musyoka (Wiper) na Jaji Mkuu Martha Koome wamehudhuria ili kusikiliza hotuba hiyo ya pamoja bungeni na ambayo ni ya nane tangu Rais Kenyatta atwae uongozi mwaka 2013.

You can share this post!

Serikali yadhamiria kuzima matumizi ya makaa, kuni katika...

Leads United inapigiwa chapuo kufanya kweli

T L