• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 8:50 AM
Rais Ruto awashauri maafisa wa KRA wawe na utu kwa walipaji wa ushuru

Rais Ruto awashauri maafisa wa KRA wawe na utu kwa walipaji wa ushuru

NA CHARLES WASONGA

RAIS William Ruto amewaonya maafisa wa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) dhidi ya kuwadhulumu Wakenya wanapoendesha wajibu wao wa kukusanya ushuru kutoka kwao (raia).

Dkt Ruto alisema raia hawafai kukosewa heshima kwa sababu pesa zinazotokana na ushuru wanaolipa ndizo zinatumiwa kuendesha shughuli za serikali.

“Maafisa wa KRA wanaweza kufanya kazi yao vizuri kwa kuwa wapole na bila kuonekana wadhalimu kwa walipa ushuru,” Rais akasema Ijumaa alipoongoza Siku ya Ushuru wa KRA katika Kaunti ya Mombasa.

Wito wa Rais umejiri siku moja baada ya mamlaka ya KRA kuomba msamaha kwa wanandoa waliodhulumiwa na maafisa wake katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta kuhusu ushuru wa vazi la harusi.

Hata hivyo, kwenye ujumbe kupitia mtandao wa kijamii wa X (zamani Twitter), KRA ilisema kuwa vazi hilo lilikuwa la thamani ya dola 2,000 za Amerika (sawa na Sh300,000).

Lakini kulingana na kanuni ya KRA, ni bidhaa zisizozidi thamani ya dola 500 (sawa na Sh75,000) ndizo msafiri anaweza kuingiza nchini bila kulipia ushuru wowote.

“Tungependa kujulisha umma kwamba wanandoa hao walilipa ushuru hitajika baada ya kuelewa kanuni zetu kuhusu ushuru. Tunawashukuru kwa ushirikiano wao,” KRA ikasema kwenye taarifa hiyo.

Juzi, kanuni hiyo mpya ya KRA ya kuwatoza ushuru wageni wanaoingiza nchini vitu vyenye thamani inayozidi dola 500 iliibua pingamizi kubwa miongoni mwa Wakenya na hata wabunge.

  • Tags

You can share this post!

Mechi za CECAFA zaanza bila Kenya

Lamu Mashariki kupata lami kwa mara ya kwanza

T L