• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 5:50 AM
Shakahola: Miili 29 yafukuliwa idadi ya waliofariki ikipanda hadi 179

Shakahola: Miili 29 yafukuliwa idadi ya waliofariki ikipanda hadi 179

NA ALEX KALAMA 

MAAFISA wanaoendeleza operesheni kwenye msitu wa Shakahola katika Kaunti ya Kilifi wamepata miili 29 mnamo Ijumaa.

Miili hiyo imepatikana baada ya maafisa hao kufukua makaburi na kutoa miili ya watu waliozikwa katika hali tatanishi kwenye shamba linalodaiwa kuwa la mhubiri tata Paul Mackenzie.

Akihutubia wanahabari katika eneo la Shakahola siku ya Ijumaa, Mshirikishi wa Pwani Rhoda Onyancha amesema kufikia sasa idadi ya watu walioaga dunia imefika 179 huku ya wale waliokamatwa ikisalia 25.

“Leo tumepata miili 29, hakuna mtu aliyeokolewa na pia hakuna mtu aliyekamatwa. Japo operesheni ya kuwatafuta manusura waliosalia ndani ya msitu bado inaendelea hadi sasa,” amesema Bi Onyancha.

Hata hivyo afisa huyo wa utawala amedokeza kuwa idadi ya familia zinazotafuta jamaa zao waliopotea imeongezeka kutoka 594 hadi 609 huku idadi ya watu waliookolewa ikisalia 72.

Wakati huo huo Bi Onyancha amesema idadi ya familia zilizokutanishwa na jamaa zao imesalia 14 huku idadi ya wale waliochukuliwa chembechembe za DNA ikisalia 93.

Idadi hiyo ya miili iliyopatikana mnamo Ijumaa ndio ya juu iliyowahi kupatikana kwa siku moja tangu kuanza kwa ufukuaji wa makaburi ya wahanga hao ambao inadaiwa walifuata mafundisho ya kupotosha kutoka kwa mhubiri Mackenzie.

  • Tags

You can share this post!

Askofu Josphat Njoroge ahimiza Wakenya wahifadhi mazingira,...

Ulinzi Starlets kuvaana na Kispeed Queens kombe la FKF

T L