• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 4:43 PM
SHINA LA UHAI: Teknolojia mpya ya CyberKnife tumaini la wanaougua kansa

SHINA LA UHAI: Teknolojia mpya ya CyberKnife tumaini la wanaougua kansa

NA PAULINE ONGAJI

MNAMO Septemba 27, 2023, Bw Benjamin Muthama,28, alianza matibabu yake ya mnururisho kuondoa uvimbe uliokuwa kati ya pua na macho yake, na ambao ulikuwa umeathiri uwezo wake wa kusikia pamoja na sehemu ya ubongo wake.

Matibabu hayo yalifanyika katika hospitali ya Rufaa ya Chuo Kikuu cha Kenyatta yaani KUTRRH na yalichukua muda wa chini ya dakika 30.

Hii ilikuwa awamu ya kwanza ya awamu tano za matibabu ambazo zilikuwa zimeratibiwa kufanyika kwa siku tano zilizofuatia, muda uliokamilika Oktoba 1.

Kufikia mwisho wa matibabu hayo, uvimbe huo ambao mwanzoni uliwatatiza madaktari kutokana na sehemu hatari ambao ulikuwa, hatimaye uliondolewa.

Bw Muthama alikuwa mgonjwa wa kwanza kupokea matibabu kutumia teknolojia mpya ya matibabu ya kansa ya CyberKnife katika hospitali ya KUTRRH.

Bw Benjamin Muthama akihutubia wanahabari baada ya kupata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Chuo Kikuu cha Kenyatta (KUTRRH). PICHA | HISANI

Cyberknife ni matibabu ya kiroboti ya picha. Matibabu haya hayahusishi upasuaji; kumaanisha kwamba mtu hatasikia uchungu na pia muda wa matibabu ni mfupi.

Bw Muthama ambaye ni mtaalamu wa programu za kompyuta, alilazimika kusubiri matibabu haya tangu mwaka wa 2021 ambapo hata familia yake ilikuwa ikiwazia kumsafirisha kuenda nchini India kwa matibabu.

“Nafurahia kwamba subira yangu hatimaye imevuta heri kwani nilitumia muda mfupi kwenye wodi ya hospitali kinyume na mambo yanavyokuwa baada ya upasuaji wa kawaida,” aongeza.

Bw Benjamin Muthama (kushoto) na babake baada ya matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Chuo Kikuu cha Kenyatta (KUTRRH). PICHA | HISANI

Matibabu haya yalifanywa na kikosi cha wataalamu wa afya ikiwa ni pamoja na wanaonkolojia, madaktari wa kawaida na wataalamu wa tiba ya mnururisho.

Kwa mujibu wa Elly Jabbour ambaye ni mtaalamu wa cyberknife kutoka Accuray, kampuni iliyounda mtambo huu kutoka Amerika, cyberknife ina uwezo wa kutoa dozi kali za matibabu kwa kipindi kifupi, ikilinganishwa na aina nyingine za matibabu ya mnururrisho.

“Kwa mfano, katika matibabu ya ubongo, utaratibu huu unahusisha awamu tano za matibabu badala ya 33 kama ilivyo kawaida,” aeleza Bw Jabbour.

Aidha, mtambo huu waweza kusonga katika vipenyo tofauti, na hivyo kutoa dozi kadhaa za mnurururisho zinazolenga sehemu husika, huku zikihifadhi tishu zinazozingira eneo lililoathiriwa.

Mbali na hayo, msukosuko wa uvimbe wakati wa matibabu unaosababishwa na kukohoa, kupumua au kumeza miongoni mwa mengine, hauathiri usahihi wa tiba hii kwani mtambo huu umesanifiwa kubadilisha miale ya mnururisho vilivyo.

“Usahihi huu hupunguza uwezekano wa tishu kuharibika, kumaanisha kwamba athari hasi zinazotokana na matibabu haya ni chache,” aongeza Bw Jabbour.

Madaktari wanaweza kutumia teknolojia hii kutibu maradhi kadhaa, ikiwa ni pamoja na uvimbe usiosababisha kansa pamoja na ule unaosababisha maradhi haya.

Kulingana na Dkt Tracy Irura, mwanaonkolojia katika hospitali ya KUTRRH, mtambo huu unaweza kufikia sehemu za mwili ambazo awali zilidhaniwa kutoweza kufikiwa, na hivyo waweza kutumika kutibu baadhi ya uvimbe na kansa kama vile ya kichwa na shingo, kongosho, tezi za uzazi, matiti, mapafu na ini, vile vile uvimbe wa ubongo na uti wa mgongo.

Matibabu haya yanagharimu kati ya Sh300,000 na 350,000 na kulingana na Prof Olive Mugenda, Mwenyekiti wa Bodi ya KUTRRH, NHIF itagharimia matibabu ambapo pia kuna mipango ya kuhusisha kampuni nyingine za bima.

Kwa mujibu wa Bw Isaac Kamau, mkurugenzi wa kituo cha Integrated molecular imaging center katika hospitali ya KUTRRH, matibabu haya yanatarajiwa kupunguza gharama za matibabu ya kansa, na hivyo kupunguza idadi ya watu wanaosaka matibabu ng’ambo.

“Kwa wagonjwa wanaosafiri kuelekea ng’ambo ili kutafuta matibabu, sasa wanaweza kupata matibabu hayo nchini mwao, kumaanisha kwamba watapunguza gharama ya usafiri na hoteli, miongoni mwa mambo mengine.”

Kila mwaka, maelfu ya Wakenya husafiri kuenda ng’ambo ili kupokea matibabu maalum na hasa dhidi ya kansa.

Baadhi ya mataifa ambayo yanapendelewa na wagonjwa kutoka humu nchini ni pamoja na India, Afrika Kusini na Uingereza. Takwimu za serikali zinaonyesha kwamba safari hizi huigharimu Kenya takriban Sh15 bilioni kila mwaka.

Mtambo wa cyberknife ni wa kwanza katika mataifa yaliyoko Kusini mwa Jangwa la Sahara, na wa pili tu barani Afrika baada ya ule wa nchini Misri.

Kutokana na hili, hospitali hii inatarajia wagonjwa si tu kutoka hapa nchini, bali sehemu nyingine barani Afrika.

Cyberknife itaweza kutibu hadi wagonjwa kumi kwa siku. Isitoshe, kuanzia mwisho wa mwezi Septemba ambapo matibabu haya yalianza kutolewa rasmi katika hospitali hii, zaidi ya wagonjwa 100 walikuwa wameratibiwa kuanza kupokea matibabu, huku wengine zaidi ya 800 wakiuliza maswali kuhusu matibabu haya.

“Tunatarajia wagonjwa hasa kutoka Afrika Mashariki na mataifa mengine barani, kumaanisha kwamba hawatalazimika kusafiri kuenda India au nchi nyingine za ng’ambo kwa matibabu. Tunatarajia kutibu kufikia wagonjwa 300 katika kipindi cha mwaka wa kwanza wa kuanza matibabu,” aeleza Bw Kamau.

Ili kujiandaa kwa ongezeko la idadi ya wagonjwa wanaotarajiwa kumiminika hospitalini humo, Bw Kamau asema kwamba wameunda mfumo wa kuwezesha wagonjwa kuwasiliana na wataalamu moja kwa moja.

“Pia, wahudumu wa afya wamepokwa mafunzo kuhusiana na matibabu haya, na tumeandaa kituo cha makazi kwa wagonjwa wanaotoka nchi nyingine.”

  • Tags

You can share this post!

Maskini Raila! Viongozi watoa sababu za kumhepa

Wito kaunti ijenge kituo cha utalii katika kijiji ambapo...

T L