• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:50 AM
FATAKI: Mabinti kufuata pesa ni sawa ila wasikae tu ndee wakitegemea jasho la wanaume

FATAKI: Mabinti kufuata pesa ni sawa ila wasikae tu ndee wakitegemea jasho la wanaume

NA PAULINE ONGAJI

NI kawaida kuwasikia baadhi ya wanaume hasa wa humu nchini wakilalama kuhusu jinsi mabinti wa siku hizi wanavyopenda pesa, jambo ambalo limefanya iwe changamoto kupata mke.

Kulingana na wanaotawaliwa na kauli hii, mabinti wengi siku hizi ni wa kuogopewa kwani hawana haja na wanaume wenye mifuko mikavu. Mabinti hawa wanatambulika kwao kama wachimba migodi, kumaanisha wanawake wanaotumia mahusiano kama kitega uchumi.

Ukweli ni kwamba mabinti wa aina hii wapo, na mara nyingi vituko wanavyowafanyia akina kaka sio haki.

Lakini nani atalaumiwa kwa viumbe wa aina hii ambao hisia zao za mapenzi zinategemea na kina cha mfuko wa dume? Yapi yaliyochangia kuchipuka kwa wanawake wa aina hii wenye nafsi zisizowasuta?

Tunaishi katika ulimwengu ambapo ni kawaida kwa mwanamume kumtema mkewe na kumwendea binti anayemdhania kuwa mrembo zaidi, pindi anapoanza kuimarika kiuchumi. Nakumbuka hivi majuzi nilisimuliwa kisa cha mwanamke aliyefukuzwa na mumewe wa miaka 18.

Hii ni licha ya kuwa bibi huyu alikuwa amejinyima na kusimama na dume hili na kuchangia pakubwa ufanisi wake kama wakili. Lakini pindi mume alipoanza kupata umaarufu na kuanza kuimarika kiuchumi, hakusita kumtaliki mkewe.

Nilishuhudia haya jirani yangu mmoja alipoamua kumtupilia mbali mkewe wa miaka mitano na kumuoa mwanamke mwingine baada ya kuimarika kifedha. Kumbuka kuwa bibi huyu alimpenda akiwa hana mbele wala nyuma.

Katika miaka ya ndoa yao, tulishuhudia mwanamke huyo akitia bidii na hata kumlisha kaka ambaye mwanzoni hakuwa na ajira. Lakini pindi jamaa alipofanikiwa na kupata ajira na hata kupandishwa madaraka, akaanza kuona udhaifu wa mkewe.

Hii ni taswira ambayo imeshuhudiwa katika mahusiano vilevile ndoa nyingi, jambo ambalo nina uhakika kwamba limewafanya mabinti siku hizi kuwa chonjo.

Vipusa hawa hawapaswi kulaumiwa kwani wanahofia jasho lao kuliwa na mwingine. Bila shaka sikubaliani na tabia ya baadhi ya wanawake wanaokaa kitako na kusubiri kuwawinda wenye mifuko mizito, kwa matumaini ya kujinasua kiuchumi ila pia, siwalaumu wasio na ile subira ya akina nyanya zetu.

Huenda wameshuhudia unyama wanaofanyiwa wanawake mikononi mwa madume fukara pindi yanapoanza kugusa senti.

  • Tags

You can share this post!

MALEZI KIDIJITALI: Teknolojia haiwezi chukua nafasi ya...

Misri, Ghana mawindoni kufukuzia nafasi ya kuingia AFCON...

T L