• Nairobi
  • Last Updated December 5th, 2023 8:55 PM
JUNGU KUU: IEBC gae Chebukati, wenzake wakistaafu

JUNGU KUU: IEBC gae Chebukati, wenzake wakistaafu

NA BENSON MATHEKA

KUANZIA Jumanne, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC), haitakuwa na makamishna kufuatia kukamilika kwa muhula wa kuhudumu wa Mwenyekiti wake Wafula Chebukati na makamishna wawili waliobaki Boya Molu na Profesa Abdi Guliye.

Muhula wa watatu hao waliokuwa katika mrengo mmoja baada ya mgawanyiko uliozuka kufuatia matokeo ya kura ya urais mwaka 2022 utakamilika rasmi Januari 17 baada yao kuhudumu kwa miaka sita.

Msururu wa matukio ya baada ya uchaguzi mkuu Agosti 9 ulipelekea kujiuzulu kwa makamishna watatu kati ya wanne waliopinga hatua ya Chebukati ya kumtangaza Rais William Ruto mshindi dhidi ya Raila Odinga wa Azimio la Umoja One Kenya.

Naibu Mwenyekiti wa tume hiyo Juliana Cherera na wenzake Francis Wanderi na Justus Nyang’aya waliamua kujiuzulu Rais Ruto alipokubaliana na Bunge na kuunda jopo la kuwachunguza.

Kiongozi wa nchi alikuwa amedai wanne hao “walihusika na jaribio la kubatilisha uamuzi wa Wakenya uchaguzini hatua ambayo ingezua taharuki nchini”.

Bi Irene Masit aliyekuwa katika mrengo wao alikataa kujiuzulu na kuamua kufika mbele ya jopo linaloongozwa na Jaji Aggrey Muchelule japo hawezi kutekeleza shughuli za tume kwa kuwa alisimamishwa kazi na Rais Ruto kabla ya kuunda jopo la kuwachunguza.

Wataalamu wa uchaguzi wanasema kwamba baada ya kuondoka kwa Chebukati na kundi lake, IEBC haitakuwa na uwezo wa kufanya uamuzi wa kisera kwa kukosa makamishna japo utekelezaji wa shughuli zingine utaendelea chini ya Afisa Mkuu Mtendaji Hussein Marjan.

Profesa Guliye anaonekana kuondoa wasiwasi kuhusu shughuli za tume bila makamishna akisema mifumo yake imeimarika katika kipindi cha miaka sita ambayo wamekuwa ofisini.

“Kwa miaka sita iliyopita, tumekuwa tukiimarisha mifumo ya tume. Ingawa nitakuwa nikistaafu katika siku chache zijazo, niko na imani kwamba tumekuwa tukiimarisha mifumo yetu kama tume,” Profesa Guliye alisema aliposimamia uchaguzi mdogo wa useneta kaunti ya Elgeyo Marakwet wiki jana.

Ingawa Bw Marjan atasimamia shughuli za kila siku za tume, kukosa makamishna kutaathiri mchakato wa utathmini wa mipaka ambao kulingana na Katiba, unapaswa kukamilika mwaka 2024.

Bila makamishna, kisheria, IEBC haitakuwa tume na kwa hivyo haitaweza kutekeleza majukumu yake ya kisheria.

Hali itakuwa sawa hata jopo la Muchelule likimwondolea lawama Bi Masit kwa kuwa idadi ya makamishna wanaotakiwa kufanya maamuzi katika IEBC ni watatu, ilivyoamua Mahakama ya Upeo katika kesi kuhusu mchakato wa kubadilisha katiba wa Mpango wa Maridhiano (BBI).

Uajiri wa makamishna wapya wa IEBC unapaswa kuanzia Bungeni kwa kuwa Rais Ruto ametangaza kuwa wazi nafasi za makamishna watatu wa IEBC.

Mapema wiki hii, Mwenyekiti wa Kamati ya Haki na Sheria ya Bunge (JLAC) George Gitonga Murugara alinukuliwa akisema kwamba watanuia kuunda kamati ya kuongoza mchakato wa kuajiri makamishna haraka ili kuokoa hali katika tume hiyo ya uchaguzi.

Haya yanajiri huku upinzani ukipinga marekebisho ya sheria ya kuajiri makamishna yanayopendekezwa na serikali ukidai Rais Ruto ana njama ya kuwa na vibaraka wake katika IEBC akilenga uchaguzi mkuu wa 2027.

  • Tags

You can share this post!

Brighton waduwaza Liverpool kwa kuipokeza kichapo cha 3-0...

KIGODA CHA PWANI: Ziara ya Raila Mombasa kulinda ngome yake...

T L