• Nairobi
  • Last Updated December 4th, 2023 8:09 PM
MIKIMBIO YA SIASA: Raila ‘aruhusu’ magavana wake kufanya kazi na Ruto

MIKIMBIO YA SIASA: Raila ‘aruhusu’ magavana wake kufanya kazi na Ruto

NA CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga amekunja mkia na kuamua kuwapa magavana wake kibali cha kufanya kazi na Serikali ya Rais William Ruto kutokana na msukumo kutoka kwa magavana hao na wafuasi wa muungano huo.

Aidha, duru zimeiambia safu hii kwamba Bw Odinga na vigogo wenzake katika muungano huo wameingiwa na hofu kwamba kwa endapo watawazuia magavana hao kushirikiana na Serikali kuu katika nyanja za maendeleo, Azimio itaendelea kupoteza umaarufu miongoni mwa raia.

“Baba amewaweka huru magavana washirikiane na serikali ya Ruto baada ya magavana hao kukaa ngumu kwamba wanataka msaada wa serikali kuu kufanikisha miradi ya maendeleo ambayo walitoa kwa wafuasi wao wakati wa kampeni. Wafuasi wetu nao wana kiu ya maendeleo baada ya ndoto ya kinara wetu ya kuingia Ikulu kukosa kutimia,” anasema mbunge mmoja wa ODM kutoka Nairobi, ambaye aliomba tulibane jina lake.

Lakina akiongea mjini Mombasa Ijumaa Bw Odinga alisema magavana waliochaguliwa kwa tiketi za vyama tanzu katika Azimio wanafanyakazi pamoja na serikali kuu kutokana na idhini ya uongozi wa muungano.

Aidha, alisema kuwa hatua hiyo ni halali kwa sababu kwa mujibu wa Katiba serikali za kaunti zinafaa kushirikia na serikali kuu katika utekelezaji wa majukumu yao kwa manufaa ya wananchi.

Bw Odinga, ambaye alikuwa ameandamana na viongozi wa Mombasa wakiongozi wa Gavana Abdulswamad Sheriff Nassir, alionya vyombo vya habari, wafuasi wa Azimio na Wakenya kwa ujumla dhidi ya kufasiri hatua ya magavana hao kuzuru Ikulu kuashiria kuwa wamegura muungano huo na vyama vilivyowadhamini uchaguzini.

“Kufanya kazi na Serikali ya Kitaifa hakumaanishi kuwa gavana amehamia chama cha UDA au Kenya Kwisha (jina sahihi ni Kenya Kwanza). Katiba inawaruhusu magavana kufanya kazi na serikali ya kitaifa kwa manufaa ya wananchi walipa ushuru. Na magavana wetu kama mheshimiwa Nassir wanaofanya kazi na Ruto wamepata ruhusa kutoka kwetu,” akasema katika ukumbi Tononoka.

Kando na Bw Nassir, magavana wengine wa mrengo wa Azimio ambao wametangaza kuwa watashirikiana na serikali ya Rais Ruto ni; Gideon Mung’aro (Kilifi, ODM), Julius Malombe (Kitui, Wiper) na Wavinya Ndeti (Machakos).

Wengine ni pamoja na; Simba Arati (Kisii, ODM), Fernandes Barasa (Kakamega, ODM), Wilber Otichillo (Vihiga, ODM) na George Natembeya (Trans Nzoia).

Gavana wa Siaya James Orengo na mwenzake wa Kisumu Peter Anyang’ Nyong’o wamehiari kufanya kazi na Serikali ya Dkt Ruto “kwa misingi ya sheria wala sio siasa.”

“Niko tayari kufanya kazi na Serikali ya Ruto kwa manufaa wa watu wangu wa Siaya ambao ni Wakenya walipa ushuru. Rais Ruto amekaribishwa hapa Siaya kuzindua miradi yoyote ya maendeleo kwa sababu yeye ni Rais wa Wakenya wote. Lakini asitumie suala hilo kunirai mimi na wakazi wa Siaya kujiunga na chama cha UDA,” akasema mnamo Desemba 22, 2022 akiwa mjini Bondo, kaunti ya Siaya.

Lakini mnamo Oktoba 2, 2022 Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga, alikwepa kuungana na Rais Ruto kwa ibada ya Jumapili katika Kanisa la AIC, mjini Homa Bay.

Badala yake Bi Wanga, alituma ujumbe akisema kuwa alikosa kumpokea kiongozi wa taifa katika ziara yake ya kwanza kaunti kwa sababu “nimebanwa na shughuli ya mafunzo kwa maafisa na madiwani wa Homa Bay, mjini Mombasa.”

Mtaalamu wa masuala ya uongozi, Barasa Nyukuri, ambaye anasema magavana wote wanastahili kufanya kazi na serikali kuu kwa sababu ngazi hizo mbili za serikali zinahudumia Wakenya.

“Kimsingi, Mpango wa Nne wa Katiba ya sasa umeweka wazi kuwa ngazi zote mbili za serikali zinapaswa kufanyakazi kwa pamoja mradi ngazi moja haiingilii nyingine. Kimsingi, serikali ya kitaifa na zile za kaunti zinawahudumia raia wale wale,” anasema.

Kwa misingi ya cheo chake kama Rais wa nchi, Dkt Ruto ndiye mwenyekiti wa baraza shirikishi la Serikali Kuu na Serikali za Kaunti, maarufu kama “Summit”.

Naye Naibu Rais Bw Gachagua ndiye mwenyekiti wa Baraza Shirikishi la Kiserikali kuhusu Bajeti (IBEC).

Mwenyekiti mwenza wa baraza hilo ni mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) Anne Waiguru.

  • Tags

You can share this post!

Ghala la kuhifadhi dawa za kaunti ya Kiambu lajengwa Ruiru

JUKWAA WAZI: Seneta Osotsi, Koech wachafuana kuhusu...

T L