• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 12:09 PM
PENZI LA KIJANJA: Kuchagua mchumba kunahitaji hekima si hisia tu

PENZI LA KIJANJA: Kuchagua mchumba kunahitaji hekima si hisia tu

NA BENSON MATHEKA

ANAWEZA kuwa na pesa na akufanye ulie kwa kutowajibika kwako, anaweza kuwa na miraba minne na aitumie kukudhulumu badala ya kukulinda, anaweza kuwa na umbo na sura nzuri lakini moyoni awe katili kupindukia.

Hivyo basi, katika harakati za kutafuta mchumba, mtu anahitaji kuwa mjanja asijipate ameangukia wrong number akidhani amepata kiosha roho wa maisha yake.

Hasa, watu wengi siku hizi hawajali tabia ya mtu, wanachofuata ni wanachopata kutoka kwake, wanapagawishwa na mavazi, umbo, magari na kiasi cha pesa wanachochotewa na anayewarushia mistari ya mapenzi.

“Kinachosikitisha zaidi ni kwamba vipusa na mabarobaro wanachangamkia wanaowanasa kwa pombe. Unapata mwanadada au barobaro anaingia boksi ya mtu anayemnunulia pombe ya pesa nyingi na kumpeleka kula uroda katika hoteli za kifahari. Majuto yanamwandama tabia halisi za kikatili za mtu au sponsa huyo zinapoanza kubainika na kuachwa kwa mataa au kulemaa pia,” asema mwanasaikolojia Brian Githu, wa Life Center, Nairobi.

Kulingana na Githu, vipusa wanapaswa kuwa makini zaidi wasiangukie mitego ya wanaume wanaowatumia kwa muda wakiwapagawisha kwa maisha ya anasa na kisha kugeuka kuwa shetani katika maisha yao.

“Sisemi mtu aoe mtaalamu wa ucheshi lakini ni muhimu kuoa na kuolewa na mtu anayekufanya ucheke na sio tu siku za mwanzo za uhusiano wetu, bali katika maisha mtakayokuwa pamoja, kukiwa kubaya au kuzuri,” asema Githu na kuongeza kuwa mtu kama huyo hakasiriki kwa muda mrefu na ni mwepesi wa kusamehe.

“Katili huwaka kwa hasira, anapenda ugomvi na anaamini suluhu ya kukosewa ni vitisho na vita, mwepuke ikiwa unataka furaha katika uhusiano wa kimapenzi na ndoa,” asema.

Mwanasaikolojia huyu asema japo pesa ni nzuri, mtu asiyejua kuzitumia vyema hawezi kuwa mume au mke mwema.

“Unapochangamkia mtu kwa sababu ya pesa za anazotumia mponde raha, jiulize kama anajua kuzitumia vyema, hasa kwa mipango ya siku zijazo. Usiangukie mtu kwa sababu ya mifuko yake mizito, ganda kwa aliye na mipango ya maisha bora ya siku zijazo kwake na familia yake,” asema.

Kuhusu wanaopagawishwa na miraba minne au wenye figa 8, Githu anasema nguvu za mwili bila hekima ni bure.

“Chagua mtu anayeweza kutumia akili kulinda maslahi yako, anayejua kupenda na kudhihirisha anakupenda kwa dhati jinsi ulivyo. Anakujali kila wakati, wakati wa hali nzuri na vinginevyo, sio anayetoweka mambo yakikwendea mrama. Ukitekwa na mambo pesa, sura na umbo, utajuta,” asema.

  • Tags

You can share this post!

JAGINA WA SPOTI: Huyu Sidi alikuwa kodriva ngangari katika...

BAHARI YA MAPENZI: Mke asilazimishwe kuacha kazi ili...

T L