• Nairobi
  • Last Updated May 22nd, 2024 5:30 PM
JURGEN NAMBEKA: Wakuu Mombasa watafute jibu kwa wanaozurura barabarani

JURGEN NAMBEKA: Wakuu Mombasa watafute jibu kwa wanaozurura barabarani

NA JURGEN NAMBEKA

KILA unapotembea katika mitaa ya jiji la Mombasa, utakutana na watu kadhaa, wanaojisakia tonge kwa kuombaomba.

Mara nyingi huwa ni watu wanaoishi na ulemavu ama wale wenye magonjwa yaliyowasababishia viungo vya mwili kuwa na mtazamo usio wa kawaida.

Cha kufadhaisha ni jinsi omba omba hao husogea magari na kunyoosha mkono , wengine wakihatarisha maisha yao. Isitoshe, abiria mara nyingi hujipata wakishtuliwa kwa omba omba hao , ambao hujitokeza kwa gari na kunyoosha mkono ili wapate msaada.

Licha ya kuwa watu hawa wana mahitaji mbalimbali, kuna umuhimu wa serikali, kutafuta njia za kuwasaidia ili wajiondoe katikati mwa jiji.

Abiria mmoja aliwahi kumaka kwa sauti akiwa katika barabara ya kuingia jijini kutoka Changamwe eneo la Sabasaba.

Alikuwa akitoa msaada kwa ombaomba mmoja aliyekuwa akisukumwa kwa kiti cha magurudumu, ghafla akaanza kuwaona wengi wakisogea pale dirishani.

Alifunga dirisha kwa fujo na kuacha kutoa msaada, akishtuliwa na idadi kubwa ya waombaji walioendelea kumwomba hela.

Akiwa mgeni jijini Mombasa, huenda hata akaogopa kumsaidia mtu aliye na mahitaji ya kweli.

Serikali ya kaunti ya Mombasa inapaswa kutafuta njia mbadala ya kukabiliana na omba omba ili wajikimu kimaisha.

Ingefaa zaidi iwapo mgonjwa anayeweza kutibiwa angetibiwa badala ya kuachwa akiomba omba barabarani ili kukidhi njaa ya siku moja.

Ingekuwa afueni iwapo wangejianzishia biashara hata kama ni ya kuuza peremende au maji.

Katika hali hii, ni rahisi kwa wahisani kuwasaidia bila kudhaniwa kuwa matapeli. Mwaka jana, askari wa kaunti ya Mombasa na polisi walikuwa wameanza kupiga doria na kuwakamata omba omba waliokuwa wakitumia ujanja kuwatapeli wapita njia.

Juhudi zilizaa matunda kwa muda na idadi yao ikapungua, ila baadaye walianza kurejea kando ya barabara.

Idadi kubwa ya waombaji hao, huenda ikawaacha waombaji halali wakipata taabu , huku matapeli wakijitajirisha kwa shughuli hiyo.

Gavana Abdulswammad Nassir anapasa kushirikiana na mawaziri wake, kutatua kero hilo kwani linaufanya mji kuwatishia hata watalii, ikikumbukwa kuwa kaunti hiyo inategemea pakubwa sekta hiyo.

Kaunti inafaa iwaondoe omba omba wasio halali au hata kupeana vibali vya kuwaruhusu kutekeleza shughuli hiyo, ili kupunguza idadi yao.

Kwenye mipango ya ajira kama ile ya Mombasa yangu, wenye uwezo na ni walemavu wapewe nafasi ya kujisakia fedha.

  • Tags

You can share this post!

Familia ya Babu Owino yakita kambi katika kituo cha polisi...

Beki Jurrien Timber aimarisha safu ya ulinzi kambini mwa...

T L