• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 12:09 PM
TAHARIRI: Tuna wajibu wa kuzuia mabadiliko ya tabia-nchi

TAHARIRI: Tuna wajibu wa kuzuia mabadiliko ya tabia-nchi

NA MHARIRI

KWENYE kongamano kuu la mabadiliko ya tabia-nchi la Umoja wa Mataifa (UN) linaloendelea Misri, wito unaotawala ni vilio vya mataifa maskini kwa yale yaliyostawi hasa kiviwanda kufidia athari za mabadiliko hayo hasa barani Afrika.

Hamna pingamizi kuwa mabadiliko ya tabia-nchi ni tatizo kubwa linaloweza kuangamiza viume-hai vyote iwapo hayatakabiliwa kwa mbinu thabiti za kisayansi.

Humu nchini, katika misimu mitatu ya hivi majuzi maeneo mengi hayajashuhudia ama mvua ya kutosha au hata kukosa kabisa.

Hali hiyo imechangia janga kubwa la njaa ambalo bila shaka limeangamiza raia wengi na mifugo.

Wala tatizo hilo halijaathiri Kenya pekee bali mataifa mengi mno ya ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara kama vile Sudan, Somalia, Ethiopia na mengineyo.

Wajumbe wengi wanaohudhuria kongamano la mwaka huu almaarufu COP27 nchini Misri, wamekuwa wakiyalaumu mataifa tajiri kama vile Amerika, China, Japan, na mengineyo ya bara Ulaya, wakiyataka yafidie hasara kubwa ambayo imesababishwa na ukame uliozuka kutokana na mabadiliko ya hali ya anga baada ya utando muhimu almaarufu Ozone Layer kuharibiwa na gesi hatari zinazotoka viwandani.

Utando huo ndio huzuia jua kali kuumiza viumbe hai duniani. Naam nasi tunawaunga mkono wajumbe hao ambao wamedai mabilioni ya pesa za kufidia uharibifu huo.

Lakini huku mataifa yanayostawi kama vile Kenya yanaposubiri fidia hiyo, ni muhimu mataifa haya yenyewe nayo yaanze kuchukua hatua madhubuti za kuhakikisha nayo yanachangia kikamilifu katika kurejesha hali nzuri ya anga.

Mojawapo ya hatua hizo ni kupanda miti kwa wingi. Ukosefu wa miti umetajwa na wataalamu kuwa sababu kuu ya kuadimika kwa mvua. Hivi majuzi serikali ya Rais William Ruto imetangaza kuwa inapanga kupanda miti bilioni moja kila mwaka.

Azimio hili hakika ni zuri nasi tunafaa kuliunga mkono.

  • Tags

You can share this post!

Tamaa itakayosukuma Ruto kubadili katiba

JUNGU KUU: Dau la Azimio laelekea kuzama

T L