• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 1:05 PM
AS Monaco waaibisha PSG katika Ligi Kuu ya Ufaransa

AS Monaco waaibisha PSG katika Ligi Kuu ya Ufaransa

Na MASHIRIKA

KOCHA Mauricio Pochettino amesema matokeo duni yaliyosajiliwa na Paris Saint-Germain (PSG) dhidi ya AS Monaco katika Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) mnamo Jumapili usiku “hayakubaliki” na “ni ya aibu katika mchezo wa soka”.

PSG ambao ni viongozi wa jedwali la Ligue 1 walizidiwa ujanja katika vipindi vyote viwili vya mchezo na kichapo cha 3-0 walichopokezwa na Monaco ndicho kinono zaidi kwa kikosi hicho kupokezwa ligini kufikia sasa msimu huu.

Matokeo hayo pia yalimaanisha kwamba PSG kwa sasa wamepoteza mechi nne kati ya sita zilizopita katika mashindano yote.

“Tulipoteza mechi kwa namna isiyokubalika kabisa hasa katika hatua hii ya kampeni za Ligue 1. Ni matokeo ya aibu kwa PSG,” akasema mkufunzi huyo wa zamani wa Tottenham Hotspur.

Wissam Ben Yedder alifungua Monaco mabao mawili na kutua kileleni mwa orodha ya wafungaji bora wa Ligue 1 kufikia sasa msimu huu kwa magoli 17, mawili zaidi kuliko Kylian Mbappe wa PSG. Bao jingine la Monaco lilifumwa wavuni kupitia Kevin Volland aliyemwacha hoi kipa Gianluigi Donnarumma.

PSG walipepetwa na Monaco siku 10 baada ya Real Madrid ya Uhispania kuwadengua kwenye hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kwa jumla ya mabao 3-2.

Kutokuwepo kwa nyota Lionel Messi kambini mwa PSG kuliweka Pochettino katika ulazima wa kutegemea zaidi maarifa ya Mbappe katika safu ya mbele.

Licha ya kushindwa, PSG wangali kileleni mwa jedwali la Ligue 1 kwa alama 65 huku pengo la pointi 13 likitamalaki kati yao na nambari mbili Rennes. Monaco wanashikilia nafasi ya saba kwa alama 44 sawa na Lens.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Siasa zazima uwezo wa serikali kuweka sheria

Wanga alia yumo hatarini mchujo ukikaribia

T L