• Nairobi
  • Last Updated December 8th, 2023 10:25 PM
Hofu ya KSSSA kuhusu michezo ya Shule za Upili

Hofu ya KSSSA kuhusu michezo ya Shule za Upili

Na GEOFFREY ANENE

KATIBU wa Shirikisho la Michezo ya Shule ya Upili Kenya (KSSSA) David Ngugi ameelezea hofu yake kuwa michezo hiyo huenda isirejee hivi karibuni.

Akikiri kuwa michezo hiyo imevurugwa kabisa na janga la virusi vya corona, Ngugi pia alielezea wasiwasi wake kuwa kizazi cha wanafunzi kitapoteza sehemu muhimu ya ukuaji wa maisha yao.

“Shughuli nyingi za michezo ya shule zimekwama ikiwemo kutambua talanta. Nahofia kuwa kizazi cha wanafunzi hakitakuwa kwenye jukwaa la michezo hii ili kunufaika na udhamini wa masomo, ajira na kadhalika,” aliongeza afisa huyo.

Ngugi alifichua kuwa KSSSA iliandaa warsha mjini Embu juma lililopita kukamilisha kulainisha masharti ya afya shule zitahitaji kutekeleza iwapo michezo hiyo itapata idhini ya serikali kuanza.

“Tunatumai kukutana na Katibu katika Wizara ya Michezo hivi karibuni kupata mwelekeo,” alisema Ngugi na kukiri kuwa hawajui michezo hiyo itarejea viwanjani lini.

“Baada ya Rais (Uhuru Kenyatta) kuongeza marufuku ya michezo na tamasha za shule kwa siku 90, tunaweza tu kuwazia kurejea viwanjani muhula ujao,” alisema.

Ngugi aliongeza kuwa hakuna hakikisho michezo hiyo itarejea uwanjani kabla ya hali ya humu nchini kuimarika. “Tusisahau kuwa kuna hofu kuhusu uwezekano wa wimbi la pili virusi vya corona.”

  • Tags

You can share this post!

Nyuki wakatiza shughuli ya kusajili makurutu KDF

Kimemia alaani ubomozi wa majengo Ol Kalou