• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Injera ashukuru Melrose 7s Scotland kumtambua kama shujaa

Injera ashukuru Melrose 7s Scotland kumtambua kama shujaa

Na GEOFFREY ANENE

NYOTA Collins Injera amesema ni heshima kubwa kutiwa katika orodha ya mashujaa wa mashindano ya Melrose Sevens uwanjani Greenyards nchini Scotland.

Injera aliyechezea Kenya kwenye Raga za Dunia kwa miaka 16 kabla ya kustaafu mwaka 2022 amesema hayo Aprili 7, siku moja baada ya kupokea tuzo hiyo katika dhifa ya usiku mjini Melrose.

Katika hafla hiyo iliyoleta pamoja wapenzi wa raga 200, Injera pamoja na wachezaji wa zamani Eric Paxton na Lisa Thomson pia walitiwa katika orodha ya mashujaa wa Melrose Sevens.

“Ni heshima kubwa na ninanyenyekea kutiwa katika orodha ya mashujaa wa Melrose Sevens hapa Melrose ambapo raga ya wachezaji saba kila upande ilizaliwa. Pongezi ziwaendee pia mashujaa wenzangu Lisa Thomson na Eric Paxton,” ameandika kwenye mitandao yake ya kijamii.

Mchezaji huyo wa zamani wa klabu za Ulinzi na Mwamba aliyeanzia safari yake ya raga katika shule ya upili ya Vihiga katika kaunti ya Vihiga, alipata umaarufu katika raga ya wachezaji saba kila upande kwa utimkaji wake na kuchenga wapinzani.

Wakati mmoja, Injera alishikilia rekodi ya mfungaji wa miguso mingi kwenye Raga za Dunia ambazo aliwahi kushinda duru ya Singapore Sevens mwaka 2016.

Msomi huyo wa masuala ya uanahabari alistaafu baada ya Kombe la Dunia 2022 nchini Afrika Kusini, akiwa na nambari mbili kwa ufungaji wa miguso (271) kwenye raga hizo za kifahari nyuma ya Muingereza Dan Norton.

Mwezi Januari 2023, Injera, ambaye aliibuka mfungaji bora wa miguso kwenye Raga za Dunia msimu 2008-2009 (miguso 42), pia alitiwa katika orodha ya mashujaa wa McDonald’s Fiji Coral Coast Sevens (RugbyTown Walk of Fame) nchini Fiji.

  • Tags

You can share this post!

Vigogo wa chess wang’aa mashindano ya Kenya Open

DOUGLAS MUTUA: Ruto na Raila watafute suluhisho kama...

T L