• Nairobi
  • Last Updated December 2nd, 2023 1:45 PM
Pigo zaidi kwa Leicester baada ya Jamie Vardy pia kupata jeraha

Pigo zaidi kwa Leicester baada ya Jamie Vardy pia kupata jeraha

Na MASHIRIKA

MSHAMBULIAJI matata wa Leicester City, Jamie Vardy anatarajiwa kusalia mkekani kwa takriban mwezi mmoja baada ya kupata jeraha la paja wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyowashuhudia wakitandika Liverpool 1-0 mnamo Disemba 28, 2021 ugani King Power.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 34 alitibiwa uwanjani baada ya kugongana na beki Joel Matip na akahiari kuendelea na mchezo hadi kipenga cha mwisho.

Jeraha la paja lililomkoseha Vardy fursa ya kuunga kikosi cha Leicester mnamo Disemba 26 waajiri wake walipopepetwa 6-3 na Manchester City ugani Etihad.

“Tutamkosa Vardy kwa wiki tatu au nne hivi,” akasema kocha Brendan Rodgers wa Leicester.

Kuumia kwa Vardy ni pigo kubwa kwa Leicester ikizingatiwa kwamba mshambuliaji mwenzake Patson Daka pia anatarajiwa kusalia nje kwa wiki mbili au tatu baada ya kupata jeraha akicheza dhidi ya Liverpool kwenye Carabao Cup. Kelechi Iheanacho na Wilfred Ndidi pia wameitwa kuunga kikosi cha Nigeria kwa ajili ya fainali za Kombe la Afrika (AFCON) kati ya Januari 9 na Februari 6, 2022.

Vardy ambaye amefunga mabao 11 kutokana na mechi 22 za hadi kufikia sasa msimu huu, anafikisha idadi ya wanasoka wa Leicester wanaouguza majeraha mbalimbali kuwa saba.

Leicester wanatazamiwa sasa kutegemea zaidi wanasoka Ademola Lookman na Ayoze Perez katika safu yao ya mbele kwa kipindi cha wiki kadhaa zijazo.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Lukaku akiri kutofurahia maisha Chelsea, adokeza uwezekano...

Boga, Kwekwe waungana kuwania ugavana Kaunti ya Kwale

T L