• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 8:11 PM
Joseph Yobo aamini Kenya ina wanasoka wenye uwezo wa kung’ara Ulaya

Joseph Yobo aamini Kenya ina wanasoka wenye uwezo wa kung’ara Ulaya

Na CECIL ODONGO

NYOTA wa zamani wa Everton Joseph Yobo anaamini kuwa Kenya ina wachezaji ambao talanta zao zikikuzwa vyema, watakuwa na uwezo wa kutamba sio tu kwa klabu za Afrika bali pia bara Ulaya.

Yobo,42,  ambaye pia alikuwa nahodha wa Nigeria mnamo Jumamosi usiku alikuwa kati ya mamia ya mashabiki ambao walitazama mechi ya Uefa kati ya Inter Milan na Manchester City kwenye runinga kubwa katika hoteli ya Emara Ole Sereni, Nairobi.

Man City ilichapa Inter Milan 1-0 na kutwaa ubingwa wa Uefa kwa mara ya kwanza katika historia yake. Yobo pamoja na Kocha wa zamani wa Harambee Stars Jacob ‘Ghost’ Mulee, mwanaspoti Njeri Meg walikuwa wachanganuzi ambao walizungumzia mechi hiyo kabla na baada ya kusakatwa kwake.

Kutoka Kushoto: Kocha Jacob ‘Ghost’ Mulee, Meneja wa Mastercard East Africa Shehryar Ali, mwanasoka nguli wa zamani aliyekuwa nahodha wa Nigeria Joseph Yobo na mwanahabari Njeri Meg kwenye hafla iliyoandaliwa na Mastercard kuwapa mashabiki wa soka fursa ya kipekee kutazama fainali ya Klabu Bingwa Ulaya kwenye runinga ya skrini kubwa jijini Nairobi. Manchester City walipiga Inter Milan 1-0 na kutwaa taji hilo. PICHA | CECIL ODONGO

Alisema kuwa wachezaji Wakenya wanaweza kufikia hadhi ya mnyakaji wa Inter Andre Onana ambaye alikuwa akinyakia Inter Milan kwenye kipute hicho kilichogaragazwa Istanbul Uturuki.

“Nimecheza dhidi ya Kenya hapo awali na pia nafahamu klabu kama Gor Mahia ambayo imekuwa ikishiriki mechi za CAF. Kutokana na uwekezaji mzuri na pia bidii, wanasoka Wakenya wanaweza kufikia hadhi ya Onana,” akasema Yobo.

Hafla hiyo ilidhaminiwa na Kampuni ya MasterCard kupitia meneja wake nchini Shehryar Ali ambaye alisisitiza kuwa wataendelea kuwafikia wateja wao hasa kupitia soka.

Yobo alichezea Everton kwa miaka minane ambapo aliwajibika uwanjani kwa zaidi ya mara 250 kabla ya kuondoka na kujiunga na Fenerbahce Uturuki mnamo 2012. Alijiunga na timu hiyo mnamo 2002 kama mmoja wa wachezaji ambao walisajiliwa na aliyekuwa kocha wa Everton David Moyes.

Alistaafu kucheza soka baada ya Kombe la Dunia mnamo 2014 baada ya kucheza zaidi ya mechi 100 kwa Nigeria.  Kwa sasa anashughulikia biashara zake na anatumai kuwa siku moja atawania Urais wa Shirikisho la Soka Nigeria.

  • Tags

You can share this post!

Kindiki: Wenye mabaa na vilabu kuomba upya leseni

Baha achukua mapumziko mafupi mitandaoni

T L