• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 11:50 AM
Klopp ataka Liverpool kujihadhari dhidi ya Inter Milan katika marudiano ya UEFA ugani Anfield

Klopp ataka Liverpool kujihadhari dhidi ya Inter Milan katika marudiano ya UEFA ugani Anfield

Na MASHIRIKA

LIVERPOOL wamepigwa jeki na kupona kwa wachezaji Roberto Firmino, Thiago Alcantara na Joel Matip wanaotarajiwa kuunga kikosi kitakachotegemewa na kocha Jurgen Klopp dhidi ya Inter Milan katika marudiano ya hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) ugani Anfield mnamo Machi 8, 2022.

Liverpool watashuka dimbani wakilenga kuendeleza ubabe uliowavunia ushindi wa 2-0 dhidi ya Inter katika mchuano wa mkondo wa kwanza mnamo Februari 16, 2022.

Firmino, 30, alifungia Liverpool bao la kwanza dhidi ya Milan katika mchuano wa mkondo wa kwanza uwanjani San Siro. Mshambuliaji huyo raia wa Brazil hajachezea waajiri wake tangu wakati huo kutokana na jeraha la paja.

Matip, 30, naye hajachezea Liverpool tangu aongoze kikosi chake kupepeta Chelsea kwa penalti 11-10 katika fainali ya Carabao Cup mnamo Februari 27, 2022. Thiago, 30, naye alipata jeraha akipasha misuli yake moto wakati wa fainali hiyo iliyozolea Liverpool taji lao la kwanza msimu huu wa 2021-22 ugani Wembley.

Licha ya Liverpool kujivunia ushindi wa 2-0 dhidi ya Inter Milan katika mkondo wa kwanza, Klopp amewataka masogora wake kutobeza mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

“Hawaji Uingereza, hasa ugani Anfield kama watalii. Watakuja kushambulia ili wakomboe na wabatilishe matokeo ya mkondo wa kwanza. Nasi hatutakaa tu kusubiri kushambuliwa. Tutashambulia na hilo ndilo tunalolitaka,” akasema mkufunzi huyo raia wa Ujerumani.

Baada ya kutwaa kombe la Carabao Cup, Liverpool wangali wanafukuzia mataji manne zaidi ukiwemo ufalme wa UEFA, ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na Kombe la FA.

Kufikia sasa, Liverpool wanashikilia nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa alama 63, sita pekee nyuma ya viongozi na mabingwa watetezi Manchester City. Nafuu zaidi kwao ni kwamba Man-City wametandaza mchuano mmoja zaidi na watakutana ugani Etihad kwa mkondo wa pili wa EPL mnamo Aprili 10, 2022.

Baada ya kutamalaki mechi zote sita za hatua ya makundi, ushindi dhidi ya Inter mwezi uliopita ulikuwa wa saba mfululizo kwa Liverpool kusajili katika gozi la UEFA muhula huu.

Iwapo watakomoa Inter kwa mara nyingine, basi Liverpool wataweka rekodi ya kuwa kikosi cha kwanza cha Uingereza kuwahi kushinda mechi nane mfululizo za kampeni za UEFA katika msimu mmoja.

Mbali na motisha ya kutaka kuweka historia ya kuwa kikosi cha kwanza cha Uingereza kuwahi kunyanyua mataji manne katika msimu mmoja, Liverpool wanajivunia rekodi ya kutoshindwa nyumbani kwa zaidi ya mwaka mmoja uliopita.

Ushindi wa 1-0 uliosajiliwa na Liverpool dhidi ya West Ham United katika mchuano uliopita wa EPL ulikuwa wao wa 12 mfululizo katika mashindano yote.

Fomyula ya pekee kwa Inter ya kocha Simone Inzaghi kutinga robo-fainali za UEFA muhula huu ni kubebesha Liverpool gunia la mabao katika gozi la Machi 8, 2022. Miamba hao wa Serie A watajibwaga ulingoni siku nne baada ya kupokeza limbukeni Salernitana kichapo cha 5-0 ligini.

Inter hawajawahi kuingia hatua ya nane-bora ya UEFA tangu 2010-11 walipotawazwa wafalme wa Serie A. Ni Manchester United pekee – dhidi ya PSG mnamo 2018-19 – ambao wamewahi kutoka chini baada ya kichapo cha mabao mawili katika mkondo wa kwanza wa UEFA na kusonga mbele katika kipute hicho.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Johana Omondi aanza maisha Ubelgiji kwa ushindi

Kocha Lennon ayoyomea Cyprus kudhibiti mikoba ya Omonia...

T L