• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
Shujaa roho juu ikielekea Malaga 7s Uhispania

Shujaa roho juu ikielekea Malaga 7s Uhispania

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande maarufu kama Kenya Shujaa ina matumaini makubwa ya kufanya vyema kwenye duru ya tatu ya Raga za Dunia mjini Malaga hapo Januari 21-23.

Vijana wa kocha Innocent ‘Namcos’ Simiyu waliratibiwa kuondoka nchini usiku wa kuamkia leo kupitia nchini Qatar. “Tulikamilisha mazoezi yetu ya hapa nyumbani ugani Kasarani mnamo Jumamosi. Tuna ari na tuko tayari kwa mashindano,” alieleza Simiyu.

Shujaa, ambayo ilimaliza mashindano mawili ya mwaliko jijini Madrid mwezi Februari 2021 ikijiandaa kwa Olimpiki, itavaana na Canada na Wales katika mechi zake mbili za kwanza za siku ya kwanza ya Malaga Sevens halafu ikamilishe Kundi D dhidi ya Ufaransa mnamo Januari 22.

Inaelekea Uhispania ikikamata nafasi ya nane kwa alama 22 baada ya duru mbili za kwanza mjini Dubai mwaka 2021 ambapo ilifika robo-fainali. Baada ya Malaga Sevens, Uhispania itaandaa Seville Sevens mnamo Januari 28-30. Raga za Dunia zinajumuisha duru 10 ambapo timu inayokamilisha msimu katika nafasi ya mwisho huondolewa kuzishiriki.

Kikosi: Nelson Oyoo (Topfry Nakuru, nahodha), Jeff Oluoch (Homeboyz), Vincent Onyala (KCB), Kelvin Wekesa (Kabras Sugar), Alvin Otieno (KCB), Herman Humwa (Kenya Harlequin), Bush Mwale (Homeboyz), Tony Omondi (Mwamba), Johnstone Olindi (KCB), Daniel Taabu (Mwamba), Levi Amunga (KCB), Derrick Ashiundu (Kabras Sugar), Billy Odhiambo (Mwamba).

You can share this post!

Padre afutwa kazi kwa kukataa kuoa

Real Madrid wacharaza Bilbao na kutwaa taji la Spanish...

T L