• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
Simbas mawindoni kulipiza kisasi dhidi ya Namibia raga ya Stellenbosch Challenge

Simbas mawindoni kulipiza kisasi dhidi ya Namibia raga ya Stellenbosch Challenge

Na GEOFFREY ANENE

Kenya Simbas inatarajiwa kuwa na kibarua kigumu itakapofufua uadui dhidi ya mabingwa wa Afrika Namibia kwenye mashindano ya raga ya wachezaji 15 kila upande ya Stellenbosch Challenge ugani Markotter nchini Afrika Kusini, leo.

Simbas ya kocha Paul Odera inaorodheshwa nafasi ya 35 duniani, nayo Namibia inapatikana katika nafasi ya 24. Takwimu za ana kwa ana pia zinaashiria Kenya itaingia mchuano huo wa nusu-fainali kama wanyonge. Imekutana na Namibia mara nane tangu 2000.

Simbas imepoteza mechi saba baada ya kupigwa vibaya ikiwemo 53-28 mara ya mwisho zilipokutana mnamo Agosti mwaka 2018. Mara moja ambayo Simbas ilivuna ushindi ni Juni 2014 ilipoduwaza miamba hao 29-22 nchini Madagascar. Simbas iko nchini Afrika Kusini kwa ziara ya majuma matatu.

Ilianza safari hiyo kwa kukung’utwa na timu ya Carling Champions 85-17 mnamo Novemba 6 jijini Pretoria. Jone Kubu na Brian Tanga walifungia Kenya miguso katika mchuano huo. Mzawa wa Fiji, Kubu, pia alichangia mikwaju miwili na penalti. Kubu pamoja na Darwin Mukidza, nahodha Daniel Sikuta na Joshua Chisanga ni baadhi ya wachezaji Simbas itategemea kutafuta ushindi mwingine dhidi ya Namibia inayojivunia wachezaji matata wakiwemo Janco Venter na Wian Conradie wanaochezea Saracens na Gloucester katika Ligi Kuu ya Uingereza, mtawalia.

Odera alipigwa jeki na kuwasili kwa wachezaji wa Kabras Sugar George Nyambua, Brian Juma, Ephraim Oduor na Joseph Odero mnamo Jumatatu iliyopita. Nyambua ni moja ya mabadiliko matano ambayo Odera amefanya katika kikosi kitakachovaana na Namibia.

Mchuano huu utatanguliwa na nusu-fainali kati ya Brazil na Zimbabwe uwanjani humo. Washindi wa nusu-fainali hizo mbili watamenyana katika fainali Novemba 20. Timu hizi zinatumia mashindano haya kujiandaa kwa mashindano ya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia 2023 nchini Ufaransa.

Kenya, Namibia na Zimbabwe zitapepetana na Uganda, Burkina Faso na Ivory Coast katika mechi za robo-fainali za Kombe la Afrika 2022 nchini Ufaransa ambazo ni sehemu za mashindano ya kuingia Kombe la Dunia 2023.

You can share this post!

Mwanafunzi wa chuo kikuu akana kumwibia afisa wa ubalozi Sh...

Mshindi wa Kundi C kati ya Italia na Uswisi kuamuliwa na...

T L