• Nairobi
  • Last Updated December 4th, 2023 7:22 PM
Uhispania kusubiri mshindi wa mechi kati ya Uingereza na Australia

Uhispania kusubiri mshindi wa mechi kati ya Uingereza na Australia

Na MASHIRIKA

VIPUSA wa Uhispania walitinga fainali ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza katika historia baada ya kupokeza Uswidi kichapo cha 2-1 kwenye nusu-fainali jijini Auckland, New Zealand.

Salma Paralluelo, 19, alitokea benchi katika kipindi cha pili na kuwaweka Uhispania kifua mbele kunako dakika ya 81. Hata hivyo, Rebecka Blomqvist, alisawazishia Uswidi katika dakika ya 88, sekunde chache kabla ya nahodha Olga Carmona kufungia Uhispania bao la ushindi.

Kichapo hicho kilishuhudia Uswidi wakidenguliwa kwenye nusu-fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya pili mfululizo.

Kwa upande wao, Uhispania sasa watakutana na Uingereza au wenyeji Australia kwenye fainali itakayosakatiwa jijini Sydney mnamo Agosti 20, 2023.

Mechi dhidi ya Uhispania ilikuwa nusu-fainali ya nne kwa Uswidi kunogesha kwenye vipute tofauti vya haiba kubwa katika miaka ya hivi karibuni. Warembo hao walitinga hatua ya nne-bora kwenye fainali za Euro 2022 na wakakubali kichapo cha 4-0 kutoka kwa Uingereza walioishia kutawazwa mabingwa.

Awali, waliridhika na nafasi ya pili kwenye Olimpiki za 2021 nchini Japan ambapo Canada iliwafunga penalti 3-2 kufuatia sare ya 1-1. Mnamo 2019, Uswidi waliambulia nafasi ya tatu kwenye Kombe la Dunia baada ya kupepeta Uingereza 2-1 nchini Ufaransa.

Iwapo wangekomoa Uhispania, ingekuwa mara ya pili katika historia kwa Uswidi kuingia fainali ya Kombe la Dunia baada ya Ujerumani kuwapepeta 2-1 mnamo 2003 nchini Amerika.

Tofauti na Uswidi, mwaka huu ni mara ya pili kwa Uhispania kushiriki Kombe la Dunia; na waliambulia nafasi ya 12 katika jaribio lao la kwanza mnamo 2019.

Walifungua kampeni za mwaka huu kwa ushindi wa 3-0 dhidi ya Costa Rica katika Kundi C kabla ya kuponda Zambia 5-0 na kukubali kichapo cha 4-0 kutoka kwa Japan. Walikung’uta Uswisi 5-1 katika hatua ya 16-bora kabla ya kupepeta Uholanzi 2-1 kwenye robo-fainali.

Uswidi walianza kampeni za Kundi G kwa ushindi wa 2-1 dhidi ya Afrika Kusini kabla ya kulaza Italia (5-0) na Argentina (2-0). Walidengua mabingwa watetezi, Amerika, kwa penalti 5-4 baada ya sare tasa katika hatua ya 16-bora kisha wakapokeza Japan kichapo cha 2-1 kwenye robo-fainali.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

  • Tags

You can share this post!

Kuwasili kwa Moises Caicedo kwawasisimua mashabiki wa...

Idadi ya watu walioangamia kwenye mkasa wa moto Hawaii...

T L