• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:50 AM
Gachagua achokoza nyuki akikamia kudhibiti Mlima

Gachagua achokoza nyuki akikamia kudhibiti Mlima

JITIHADA za Naibu Rais Rigathi Gachagua kupigania kutawazwa kuwa kinara wa kisiasa wa eneo la Mlima Kenya zimemzolea marafiki na maadui tele kote nchini.

Bw Gachagua ambaye amejitawaza kuwa mtetezi wa maslahi ya wakazi wa Mlima Kenya, amekuwa akipambana na viongozi ‘wanaotishia’ biashara na masilahi yao.

Mnamo Desemba 20, 2022, Bw Gachagua alimfokea Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja kwa kutishia kuhamisha matatu na mabasi ya masafa marefu kutoka katikati mwa jiji la Nairobi.

“Mimi ndiye nilisihi watu wa Mlima Kenya kumpigia kura Gavana Sakaja. Hatua yake ya kuondoa matatu katikati mwa jiji la Nairobi hatutaikubali,” alisema Bw Gachagua alipokuwa akizungumza katika Kaunti ya Nyeri.

Viongozi kadhaa wa Mlima Kenya, akiwemo Seneta wa Nyeri Wahome Wamatinga na mbunge wa Githunguri Gathoni Wamuchomba, pia wamejitokeza kuunga mkono Bw Gachagua huku wakimtaka Gavana Sakaja ‘kukoma kuhangaisha wafanyabiashara wa Mlima Kenya’.

Bw Sakaja, hata hivyo, juzi alishikilia kuwa ataendelea na mpango wake wa kufurusha matatu katikati mwa jiji – hatua ambayo huenda ikasababisha uhusiano baina yake na Naibu Rais Gachagua kuzorota zaidi.

“Rais Ruto ananiunga mkono hivyo mpango huo utaendelea. Kuna watu wanapiga vita mabadiliko, lakini hatutishiki. Nairobi inashindana na majiji yaliyoendelea duniani kama vile New York, hivyo mabadiliko ni lazima,” akasema Bw Sakaja.

Magavana James Orengo (Siaya), Fernandes Barasa (Kakamega) na Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (Cotu) Francis Atwoli ni miongoni mwa viongozi ambao wamejitokeza kukemea Bw Gachagua kwa ‘kuingilia’ majukumu ya Gavana Sakaja.

“Gavana Sakaja alichaguliwa na Wakenya kutoka maeneo yote ya nchi. Kukiwa na changamoto, anashauriana na Rais Ruto na wala si Bw Gachagua,” akasema Bw Orengo.

“Bw Gachagua, koma kuingilia majukumu ya Gavana Sakaja. Alichaguliwa na wakazi wa Nairobi kuwahudumia na wala si kulinda masilahi ya wachache,” akasema Gavana Barasa.

Mbunge wa Bumula, Jack Wamboka ametishia kuwasilisha Bungeni hoja ya kutaka Bw Gachagua atimuliwe ‘kwa kugeuka mtetezi wa eneo la Mlima Kenya badala ya kutumikia Wakenya wote’.

Japo majibizano baina ya Naibu wa Rais na Bw Sakaja yamefasiriwa kuwa vita baridi kati ya Bw Gachagua na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, baadhi ya wadadisi wanapinga dhana hiyo.

“Mvutano kati ya Naibu wa Rais na Gavana Sakaja hauna uhusiano na ubabe kati ya Mabw Gachagua na Mudavadi. Ukweli ni kwamba, Bw Gachagua anajipigia debe ili awe kinara wa kisiasa wa eneo la Mlima Kenya kabla ya 2027,” anasema Bw Javas Bigambo, mdadisi wa masuala ya kisiasa.

Kulingana na Bw Bigambo, Naibu wa Rais Gachagua analenga kuhakikisha kuwa, Rais Ruto anapitia kwake ili kupata kura za watu wa Mlima Kenya 2027.

“Katika uchaguzi wa 2022, Dkt Ruto alienda moja kwa moja kwa wakazi wa Mlima Kenya kuomba kura bila kupitia kwa kinara wao wa kisiasa Rais Uhuru Kenyatta. Lakini Bw Gachagua anataka awe ndiye wa kutoa mwelekeo 2027,” anasema.

Iwapo Rais Ruto atapitia kwa Bw Gachagua kupata kura katika eneo la Mlima Kenya, Bw Bigambo anasema, atasisitiza kupewa nusu ya serikali – hatua itakayomsaidia kujipanga vyema kuwania urais 2032.

Jana Ijumaa, Bw Gachagua alionekana kuridhishwa na juhudi zake za kuvutia eneo la Mlima Kenya upande wake.

“Mlima umetulia, uko imara na mbele iko sawa,” Bw Gachagua aliandika katika ukurasa wake wa Facebook baada ya kufanya maombi alfajiri huku akitazama Mlima Kenya katika Kaunti ya Nyeri.

Naibu wa Rais aliamka alfajiri kutoka hoteli ya Fairmont Mount Kenya Safari Club ambapo viongozi wakuu serikalini wamekuwa na kongamano kujadili mikakati ya maendeleo, na kwenda ‘kuombea Kenya pamoja na Rais William Ruto’ huku akitazama Mlima Kenya.

Baadhi ya wazee kutoka eneo la Mlima Kenya sasa wanataka Rais Mstaafu Kenyatta kukabidhi mkoba wa uongozi wa eneo la Mlima Kenya kwa Bw Gachagua.

Rais Mstaafu Kenyatta alikabidhiwa vifaa vya kitamaduni – upanga, kigoda, kofia, kisu, vazi la kitamaduni, sindano – kuashiria kuwa yeye ndiye kinara wa eneo la Mlima Kenya katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Bomas miezi michache kabla ya uchaguzi wa 2013.

Vifaa hivyo, vilikuwa vimekabidhiwa kwa Mzee Jomo Kenyatta lakini vilirudishwa kwa wazee na Mama Ngina Kenyatta kufuatia kifo cha Rais wa Kwanza wa Kenya mnamo 1978.

Baadhi ya viongozi katika eneo la Mlima Kenya wanapinga vikali juhudi za Bw Gachagua kutaka kumrithi Rais Mstaafu Kenyatta kama kinara wa kisiasa wa eneo hilo.

“Ili Bw Gachagua akubalike kuwa kinara wa siasa za Mlima Kenya, ni lazima amheshimu Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta. Hii tabia yake ya kutumia kila jukwaa kumshambulia Rais Mstaafu inafanya umaarufu wake kudorora badala ya kuongezeka,” asema mshirikishi wa Baraza la Wazee Murang’a Bw Kiarie Rugami.

Aliyekuwa Gavana wa Murang’a, Bw Mwangi wa Iria anasisitiza kuwa Bw Gachagua hafai kutawazwa kuwa kinara wa Mlima Kenya.

Ripoti za Francis Mureithi, Mwangi Muiruri na Winnie Onyando

  • Tags

You can share this post!

DOUGLAS MUTUA: Tanzania inahitaji katiba mpya, si hisani ya...

Ghala la kuhifadhi dawa za kaunti ya Kiambu lajengwa Ruiru

T L