• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
Junet amkataa Wanjigi

Junet amkataa Wanjigi

Na CHARLES WASONGA

MKURUGENZI wa uchaguzi katika ODM Junet Mohamed amesema kuwa hana habari kwamba mfanyabiashara Jimmi Wanjigi anasaka tiketi ya ODM kuwania urais 2022.

Akiongea katika kipindi cha JKL katika runinga ya Citizen Jumatano usiku, Bw Mohamed ambaye ni Mbunge wa Suna Mashariki alisema ni magavana Wycliffe Oparanya (Kakamega) na Hassan Joho ndio walituma maombi ya kutaka wateuliwe kuwa kupeperusha bendera ya urais ya ODM.

“Sina habari kwamba Wanjigi pia anapania kuwania urais kwa tiketi ya chama chetu, nasikia kutoka kwako kwa mara ya kwanza. Watu ambao najua wameonyesha nia na kulipa ada ya uteuzi ni Joho na Oparanya,” Bw Mohamed akamwambia msimamizi wa kipindi hicho Jeff Koinange.

Kulingana na Mbunge huyo wa Suna Mashariki ni wawili hao ambao walilipa Sh1 milioni zinazohitajika kwa Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi (NEB) ya ODM. Hata hivyo, mbunge huyo ambaye pia ni kiranja wa wachache katika bunge la kitaifa hakufichua ikiwa kiongozi wa ODM Raila Odinga pia amelipa ada hiyo ya Sh1 milioni.

Bw Mohamed alisema NEB inatarajia kutumia mbinu ya mwafaka katika kuteua mwaniaji wa urais kwa tiketi ya ODM. Alisema hayo siku moja kabla ya Bw Odinga kutarajiwa kutangaza rasmi, katika mkutano mkubwa Karasani, kwamba atawania urais.

Mnamo Julai mwaka huu, magavana Joho (Mombasa) na Oparanya (Kakamega) walitangaza kujiondoa katika kinyang’anyiro cha urais na kuahidi kuunga mkono azma ya Bw Odinga. Kwa upande wake, Bw Wanjigi ambaye ni mfanyabiashara tajiri amekuwa akifanya ziara sehemu mbalimbali nchini kuvumisha azma yake ya urais.

Katika mikutano yake, amekuwa akifungua afisi za ODM haswa katika maeneo ya Rift Valley na Mlima Kenya huku akitoa wito kwa ODM kuendesha mchujo kwa njia huru na haki.

You can share this post!

Wanajeshi wa Ulinzi Warriors watupia jicho Ferroviario...

20 kuwania taji la Guru Nanak Rally msimu ukifika kilele

T L