• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
Makabiliano ya Joho na Kingi yafufuka upya

Makabiliano ya Joho na Kingi yafufuka upya

VALENTINE OBARA NA ALEX KALAMA

GAVANA wa Mombasa, Bw Hassan Joho, amefufua malumbano makali dhidi ya mwenzake wa Kilifi, Bw Amason Kingi, kuhusu udhibiti wa siasa za Pwani.

Huku Kinara wa ODM, Bw Raila Odinga, akianzisha mipango ya kuzuia ngome yake ya Kilifi kuyumba, mivutano ya kale kati ya magavana hao wawili imeanza kujitokeza upya.

Wawili hao ambao wanatumikia kipindi cha mwisho cha ugavana kikatiba, walikuwa na ushirikiano katika chaguzi zilizopita na kuwezesha ODM kudumisha umaarufu wake wa miaka mingi katika ukanda wa Pwani.

Hata hivyo, hatua ya Bw Kingi miaka michache iliyopita kupinga ODM na kuanzisha mipango ya kuunda chama kilicho na mizizi yake Pwani ilifanya kuanze kuwa na migogoro kati yao.

Bw Kingi aliunda Chama cha Pamoja African Alliance (PAA), ambacho mapema wiki hii kilihama Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya kuelekea kwa Kenya Kwanza, inayoongozwa na Naibu Rais William Ruto.

Bw Odinga na Bw Joho waliongoza kikosi cha wanasiasa wa ODM Kilifi kwa kampeni za siku mbili tangu Jumatano, katika hatua iliyoonekana kulenga kuzuia ufuasi wake kudidimia kuelekea kwa uchaguzi mkuu ujao.

Akizungumza akiwa Malindi, Bw Joho alimkosoa Bw Kingi kwa kuungana na Dkt Ruto, akisema Kilifi na Pwani kwa jumla imekuwa mshirika katika ODM kwa muda mrefu na haitakuwa busara kuchukua mwelekeo tofauti wakati huu.

“Wakati ODM ilipoundwa, tuliwekeza kwa hali na mali. Huwezi kujenga nyumba, ikamilike kisha wakati unataka kuingia unaambiwa uhame. Miaka hiyo yote Raila akihesabiwa, Pwani pia inahesabiwa. Sasa nishaona Raila amekaribia Ikulu waniambia nihame, niende wapi?” akasema Bw Joho.

Katika uchaguzi uliopita, ODM ilishinda viti vyote vya kisiasa Kilifi na idadi kubwa zaidi ya madiwani.

Wakati Bw Kingi akijiunga na Kenya Kwanza, Dkt Ruto alimsifu akisema umaarufu wake na weledi wa kisiasa ndio uliwezesha ODM kupata matokeo hayo bora na kueleza matarajio kwamba hali itakuwa hivyo kwa muungano wake katika uchaguzi ujao.

Hata hivyo, Bw Odinga jana Alhamisi alipuuzilia mbali dhana hiyo na kudai umaarufu wa Bw Kingi ulitokana na kuwa alikuwa mshirika wa ODM.

Huku akisimulia jinsi alivyomwongoza kisiasa tangu alipojitosa kwa ubunge Magarini katika uchaguzi wa 2002, waziri huyo mkuu wa zamani alisema uamuzi wa Bw Kingi ni usaliti kwake na kwa ODM.

“Kwa uchaguzi uliopita, Kilifi ilikuwa nambari moja kwa ushindi ODM. Kwa hivyo Kilifi imekuwa ngome ya ODM na ninataka kuona imebaki hivyo. Jenerali aliyesimamia Kilifi aliitwa Amason Jeffa Kingi. Amenipa mateke ya punda. Sasa nataka nyinyi watu wa Kilifi mumpe kichapo (uchaguzini) kuliko ile mateke ya punda,” akasema Bw Odinga.

Mbali na hatua ya Bw Kingi, umaarufu wa ODM katika kaunti hiyo ulikuwa umeanza kuyumba wakati baadhi ya wabunge na madiwani walipoamua kuegemea upande wa Dkt Ruto miaka michache iliyopita.

Wakiongozwa na Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, wengi wao baadaye walijiunga na Chama cha United Democratic Alliance (UDA), ambacho wamepanga kukitumia kuwania viti mbalimbali katika uchaguzi ujao.

Viongozi wa Azimio wamepanga kuendeleza mikutano ya kisiasa katika kaunti nyingine za Pwani ikiwemo Kwale na Mombasa hadi kesho Jumamosi.

  • Tags

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Ruto awe na msimamo thabiti kuhusu SGR

Karua, Mudavadi wapendwa zaidi kwa unaibu rais

T L