• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
Mwanawe Ruto atetea ‘afisi ya bintiye rais’

Mwanawe Ruto atetea ‘afisi ya bintiye rais’

NA BENSON MATHEKA

MWANAWE Rais William Ruto, Bi Charlene Ruto, amefafanua kwamba hatumii pesa za serikali kufadhili shughuli za afisi yake anayoita ‘Afisi ya Binti wa Taifa.’

Akiwajibu Wakenya waliomkosoa kwenye mitandao ya kijamii kwa kutangaza kuwa ana ‘Afisi ya Binti wa Taifa’, Bi Charlene alisema shughuli za afisi hiyo ni za kibinafsi na hazifadhiliwi kwa njia yoyote na pesa za mlipa ushuru.

Alisisitiza kuwa ameanzisha afisi hiyo lakini sio ya umma au kikatiba, bali ni yake binafsi na anaifadhili.

“Afisi ya Binti wa Taifa ni ya kibinafsi. Sio afisi ya kikatiba na wala haifadhiliwi na walipa ushuru wa Kenya,” Charlene ambaye ni mtaalamu wa mawasiliano alisema kwenye taarifa.

“Afisi hiyo inaendesha shughuli na mipango inayoendeshwa na Bi Charlene Ruto,” aliongeza.

Bi Charlene alifafanua kuwa, kupitia muundo wake huru, na wawezeshaji, afisi hiyo imekuwa ikizungumza na wadau kote nchini na nje ya nchi, kuhusiana na malengo yake aliyosema ni kuendeleza ajenda zinazohusu vijana na mabadiliko ya tabia nchi.

Bi Charlene Ruto amekuwa akizuru maeneo mbali mbali nchini kukutana na viongozi tofauti kujadiliana kuhusu masuala yanayofungamana na ajenda zake.

Baadhi ya kaunti ambazo ametembelea kufikia sasa ni Kitui, Embu, Tharaka Nithi, Kirinyaga na Isiolo.

Alisema kwamba, Afisi ya Binti wa Taifa kila wakati imekuwa na nia njema ya kuhakikisha vijana wa Kenya wanasikika na kupata nafasi za kuwawezesha kujikimu.

“Afisi ya Binti wa Taifa imekuwa kila wakati na nia njema ya kuhakikisha kwamba, sauti za vijana wa Kenya zinasikika na kwamba, wanapata nafasi za kuwafanya wajikimu kimaisha,” alisema.

Binti huyo wa rais, alilazimika kutoa taarifa hiyo baada ya Wakenya kukosoa hatua yake ya kuanzisha afisi hiyo.

Baadhi walichukulia hatua hiyo kama ubadhirifu wa pesa za umma kwa kuwa haitambuliwi katika katiba.

Katika video aliyotoa majuzi, Charlene alionekana akihutubia hadhira katika kongamano moja nje ya nchi na akatambulisha kikosi alichoandamana nacho akisema kinatoka afisi yake.

“Kabla ya kuendelea, ninataka kutambulisha haraka timu yangu kutoka Kenya. Kwa hivyo, nitaanza kutoka nyuma. Huyu ni Mike Sagana, ni mmoja wa wanachama wa timu yangu. Ni mwanasiasa na mshauri mkuu katika afisi yangu. Na huyu ni Jermaine Momanyi, ndiye mkuu wa masuala ya biashara na uwekezaji katika Afisi ya Binti wa Taifa,” Bi Charlene Ruto alisema.

Ni video hiyo iliyozua hisia kali zilizomfanya Bi Charlene kufafanua maana na shughuli za afisi yake.Alisema kwamba, Katiba ya Kenya haitambui Afisi ya Binti wa Taifa na hakuna vile inaweza kufadhiliwa na pesa za mlipa ushuru.

Vile vile, binti huyo wa kiongozi wa nchi amekuwa akizuru kaunti mbalimbali nchini pamoja na baadhi ya mataifa ya kigeni.

Wiki mbili zilizopita, Charlene alizua mdahalo kwa kusema kwamba alipokuwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Daystar, alikuwa akiuzia wanafunzi wenzake smokies na kachumbari.

Baadhi ya waliokuwa wanafunzi wenzake katika chuo hicho walimuunga mkono wakisema alifanya biashara hiyo licha ya baba yake kuwa naibu wa rais wakati huo.

  • Tags

You can share this post!

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Ufaransa wacharaza Morocco 2-0 na...

MAPISHI KIKWETU: Tambi za karanga za ufuta

T L