• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 9:11 AM
Washirika Azimio kumnyima Raila usingizi akipita

Washirika Azimio kumnyima Raila usingizi akipita

NA JUSTUS OCHIENG

MGOMBEA urais wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya anakabiliwa na kibarua kigumu cha atakavyowatuza washirika wake katika serikali yake, hasa baada ya kuungwa mkono na vyama vingi vya kisiasa, akifaulu kuingia ikulu.

Ingawa kuungwa mkono na vyama vingi kunamsaidia kuzoa kura katika maeneo muhimu, maslahi tofauti ya washirika wake wanaomezea mate nyadhifa serikalini yanaweza kubadilisha kampeni yake kuwa Mnara wa Babeli.

Huenda Bw Odinga alifaulu kutuliza uasi uliofuatia uteuzi wa kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua kuwa mgombea mwenza wake.Kurejea kwa kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, ambaye alikuwa ametishia kujiondoa na kugombea urais kulipiga jeki kampeni za Bw Odinga.

Hata hivyo, kulikuwa na gharama yake: Bw Odinga ameripotiwa kumuahidi Bw Musyoka nafasi tano za uwaziri ukiwemo ule wa Mkuu wa Mawaziri.

Hii inapunguza nguvu ambazo Bw Odinga atakuwa nazo akishinda na kuunda serikali kwa sababu, tayari ametoa nafasi zingine sita za uwaziri kati ya jumla ya nafasi 22 za mawaziri.

Hii inamaanisha kuwa nusu ya nafasi za uwaziri tayari zimechukuliwa hata kabla ya kufikiria atakazopatia upande wa Rais Kenyatta.

Bw Odinga anatarajiwa kudumisha mawaziri muhimu katika baraza la mawaziri la Rais Kenyatta na tayari ametangaza baadhi ya atakaoteua.

Taifa Leo imebaini kuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i, wenzake wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) Joe Mucheru na James Macharia wa uchukuzi huenda wakawa katika baraza la mawaziri la Bw Odinga.

Bw Matiang’i na Bw Mucheru wamekuwa wakishambuliwa na Dkt Ruto kuhusiana na madai ya kutumia nyadhifa zao zenye nguvu kumpigia debe Bw Odinga.

Bw Odinga pia ameahidi kudumisha Peter Munya kama waziri wa Kilimo. Inasemekana waziri mkuu huyo wa zamani ameahidi Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa wadhifa mkubwa katika serikali yake.

Aidha, ameteua manaibu wake katika ODM Hassan Joho na Wycliffe Oparanya mawaziri wa Ardhi na Fedha mtawalia huku Bi Karua akitengewa wadhifa wa waziri wa Haki na Masuala ya Katiba iwapo wataunda serikali.

Waliomezea mate wadhifa wa mgombea mwenza katika muungano wa Azimio wapatao 10 nao watakuwa wakitarajia awateue katika serikali yake.

Miongoni mwao ni aliyekuwa mbunge wa Gatanga Peter Kenneth na Mwakilishi wa Kike Kaunti ya Murang’a, Sabina Chege ambaye hatetei kiti chake.

Ingawa Seneta wa Baringo Gideon Moi, Gavana wa Kitui Charity Ngilu na mwenzake wa Nakuru Lee Kinyanjui, wanatetea viti vyao, huenda wakamfanya Bw Odinga kujikuna kichwa zaidi wakikosa kuhifadhi viti hivyo.

Kulingana na mwenyekiti wa ODM John Mbadi, hakuna kinachomzuia Bw Odinga kudumisha baadhi ya mawaziri katika serikali yake.

Mchanganuzi wa siasa Dismas Mokua anasema iwapo Bw Odinga hatatimiza matarajio ya viongozi wa vyama tanzu, anaweza kukabiliwa na hali ngumu ya kisiasa.

  • Tags

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Numerical Machining Complex isiwe tu ya...

Wadau wa sekta ya utalii wataka Uhuru kuinusuru kabla...

T L