• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 6:24 PM
PAUKWA: Ajabu ya Tundu ‘mfu’ kuwatokea wanakijiji

PAUKWA: Ajabu ya Tundu ‘mfu’ kuwatokea wanakijiji

NA ENOCK NYARIKI

MOYO wa Bwana Farijala uling’oka alipoona upindo wa nguo ya mwanawe kwenye mshumbi uliokuwa umetengenezwa na ndovu kwenye shamba la migomba.

Wingu zito la simanzi lilitanda kote katika kiambo chake.

Mzee Farijala alijilaumu kwa kupuuza wito wa mwanawe usiku uliotangulia wakati alipopiga kamsa akiomba msaada.

Lakini angejuaje kwamba kamsa ya Tundu haikuwa ya kuwachezea shere alivyokuwa amezoea?

Mkewe Farijala aliwaongoza wanawake waliofurika nyumbani kwake ili kumpa mkono wa faraja.

Mzee Hekima alipowakaribia wazee waliokuwa wamelitazama ‘kaburi’ la Tundu kwa huzuni, alipiga alnacha na kuibuka na wazo.

“Bwana Farijala, ingia ndani ya nyumba utuletee nyuma na sepetu. Tuna kazi ya kufanya. Ima fa ima tutaufukua mwili wa mtoto wetu ili tumzike kwa heshima!’’ Mzee Hekima alisema.

Nyuma na sepetu zililetwa. Vijana walioungana na wazee walichukua nyuma wakaanza kuchimbua lile shumbi la udongo ambalo liliwawia gumu na kuwachukua muda kulifukua kwa kuwa lilikuwa limetandazwa kwa kwato za tembo.

Shughuli ile ilipokuwa ikiendelea, mara Tundu alitokea mtoni huku akitetemeka kwa mzizimo wa baridi ya usiku kucha. Kuonekana kwake kulikuwa kioja kingine ambacho nusura kiwafanye waliokuwa wakilichimbua kaburi lake kuchana mbuga.

Tundu alisimulia yale yaliyokuwa yamemkumba usiku uliotangulia kwa umati uliokusanyika nyumbani kwao.

Aliomba msamaha kutokana na tabia yake ambayo iliishia kumponza hata wakati ambapo alihitaji msaada wa kila mmoja.

You can share this post!

WANTO WARUI: Serikali itumie kawi ya jua kufanikisha elimu...

MWALIMU WA WIKI: Mwinyi ‘Masharubu’ ni mwalimu tosha!

T L