• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Uhispania kumenyana na Croatia katika 16-bora baada ya kuponda Slovakia

Uhispania kumenyana na Croatia katika 16-bora baada ya kuponda Slovakia

Na MASHIRIKA

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

UHISPANIA walivuna ushindi wao wa kwanza kwenye fainali za Euro kwa kuwaponda Slovakia 5-0 katika mchuano wa mwisho wa Kundi E mnamo Juni 23, 2021 uwanjani La Cartuja, Seville.

Ushindi huo uliwawezesha Uhispania waliotawazwa mabingwa wa Euro 2008 na 2012 kukamilisha kampeni za Kundi E katika nafasi ya pili na hivyo kujikatia tiketi ya kuvaana na Croatia kwenye hatua ya 16-bora. Uhispania ya kocha Luis Enrique watajitosa ugani kwa ajili ya mchuano huo wa hatua ya muondoano wakiwa na kiu ya kuendeleza ubabe walioudhihirisha kwenye safu yao ya mbele dhidi ya Slovakia.

Mabao ya miamba hao waliotawazwa wafalme wa dunia mnamo 2010 yalifumwa wavuni kupitia Aymeric Laporte, Pablo Sarabia na Ferran Torres baada ya Martin Dubravka wa Newcastle United kujifunga kwa upande wa Slovakia.

Dubravka aliyekuwa ameokoa penalti ya Alvaro Morata, alipangua mpira uliombabatiza kabla ya kujaa ndani ya nyavu zake dakika chache baada ya kombora la Sarabia kugonga mwamba wa goli. Juraj Kucka alizamisha kabisa chombo cha Slovakia baada ya kujifunga mwishoni mwa kipindi cha pili.

Mechi kati ya Uhispania na Croatia waliokuwa wanafainali wa Kombe la Dunia mnamo 2018 nchini Urusi, sasa itachezewa jijini Copenhagen, Denmark mnamo Juni 28, 2021.Uhispania walishuka dimbani kumenyana na Slovakia baada ya kuambulia sare dhidi ya Uswidi na Poland kwenye mechi mbili za ufunguzi wa Kundi E.

Walikamilisha kampeni za kundi lao katika nafasi ya pili kwa alama tano, mbili nyuma ya viongozi Uswidi. Slovakia waliambulia nafasi ya tatu kwa alama tatu huku Poland wakivuta mkia kwa pointi moja pekee.

 

  • Tags

You can share this post!

Mpango wa Tottenham kuajiri kocha Julen Lopetegui wa...

Ronaldo afikia rekodi ya ufungaji bora wa mabao kimataifa