• Nairobi
  • Last Updated June 1st, 2023 12:23 AM
Kura: Baadhi ya kampuni Industrial Area zaruhusu wafanyakazi waende likizo

Kura: Baadhi ya kampuni Industrial Area zaruhusu wafanyakazi waende likizo

NA SAMMY KIMATU

BAADHI ya wafanyakazi katika Eneo la Viwandani kaunti ya Nairobi watakuwa na likizo ndefu baada ya wamiliki wa kampuni kufunga kazi kupisha uchaguzi wa Agosti 9, 2022.

Taifa Leo imebaini kwamba tayari kuanzia jana kampuni nyingine zimefunga kazi na kuwapa ruhusa wafanyakazi kwenda nyumbani.

Bw Galgallo Guyo, 60, mlinzi katika kampuni moja iliyoko mkabala wa barabara ya Lunga Lunga alisema wamiliki wengine wa kampuni hizo na ambao ni raia wa kigeni wamesafiri.

Aliongeza kwamba baadhi ya kampuni tayari zimefunga milango. Zile zinazopanga kufunga wiki ijayo ni za plastiki, za vyuma na za usafirishaji bidhaa.

Hata hivyo, gereji zimefunguliwa katika maeneo ya Viwandani kwa jumla.

Vilevile, Bw Guyo alieleza kwamba mbali na kufunga kazi, baadhi ya kampuni zimechukua tahadhari ambapo mabati na chuma zimechomelewa kwenye malango ya kampuni kudhibiti usalama.

“Kila wakati kuna uchaguzi mkuu nchini, milango ya kuingia katika kiwanda hufungwa kwa kufuli kisha mabati ya chuma huchomelewa upande wa nje na kufunika milango hadi siku ya kufunguliwa baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa rasmi,“ Bw Mulandi Makumi akasema.

Katika kampuni moja Viwandani, kaunti ndogo ya Makadara, wafanyakazi wamearifiwa kupitia kwa notisi ya barua kwamba watapewa ruhusa ya kwenda nyumbani kutoka Agosti 8, 2022 na kurudi kazini Agosti 15, 2022.

“Notisi ilituaraifu kwamba hatutakuwa kazini kutoka Agosti 8 nwezi huu hadi Agosti 15 kwa ajili ya shughuli ya kupiga kura,” mhasibu katika kampuni noja ya plastiki akasema.

Juhudi zetu kupata kauli ya waziri wa Leba, Bw Simon Chelugui hazikufanikiwa kwani hakujibu simu na jumbe zetu.

Vilevile, hatukuwapata katibu mkuu wa Chama cha kutetea Maslahi ya Wafanyakazi Nchini (COTU) wala naibu wake mtawalia, Mabw Farancis Atwoli na Benson Okwaro.

  • Tags

You can share this post!

GWIJI WA WIKI: John Kinyua

USHAURI NASAHA: Yazue mabadiliko chanya masomoni mwako...

T L