• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
Mwilu akemea ongezeko la ubakaji watoto

Mwilu akemea ongezeko la ubakaji watoto

NA KENYA NEWS AGENCY

NAIBU Jaji Mkuu, Philomena Mwilu, amelalamikia ongezeko la visa vya dhuluma za kimapenzi nchini, pamoja na wazazi wanaoshirikiana na watu wengine katika jamii kuficha uozo huo.

Alisema wengi huficha visa hivyo ili “kudumisha hadhi” za familia zao.

Akihutubu alipoongoza hafla ya kusherehekea Siku ya Mtoto wa Kiafrika katika Shule ya Msingi ya Mbagathi, jijini Nairobi, Jaji Mwilu alisema kuna mtindo unaoibuka, kwamba wakati mtoto anaporipoti suala la dhuluma za kimapenzi kwa wazazi wake, wazazi hao hufanya kila wawezalo kuficha visa hivyo badala ya kuweka juhudi za kuwatafutia haki wanao.

“Mzazi anayeficha visa kama hivyo hafai kuitwa mzazi. Ni aibu kubwa kwa mzazi yeyote anayeficha maovu hayo badala ya kuwasaidia wanao kupata haki!” akasema Jaji Mwilu, akiongeza kuwa watoto wengi wanaopitia dhuluma hizo hukumbwa na matatizo mengi ya kisaikolojia baadaye.

“Jamii ambayo huwa haitilii maanani maslahi na usalama wa watoto wake haifai kuwepo,” akaongeza.

Aliwaambia watoto wanaopitia dhuluma kama hizo kutonyamaza hata kidogo.

“Msinyamaze! Hata ikiwa wazazi wako hawataki kueleza jambo hilo, tafuta mtu mwingine unayemwamini na kumwambia. Inaweza kuwa ni mwalimu wako, shangazi au mtu mwingine unayemwamini-mwambie bila kuogopa. Msikubali kuwa sehemu ya wale wananyamazia maovu hayo, kwani hilo huwa kama kuwapa wahusika nafasi na ushujaa zaidi kuendelea kufanya hivyo. Msitishike hata baada ya waovu hao kuwatisha dhidi ya kuwafichua na kutafuta haki,” akaeleza.

“Kinachofanyika si kosa lako,” akasema, alipokuwa akijibu swali kutoka kwa mwanafunzi.

Mwanafunzi huyo alitaka kujua sababu inayofanya waathiriwa wa maovu hayo kuagizwa kutoa ushahidi kuhusu yaliyofanyika mahakamani, jambo ambalo huwasumbua kimawazo.

Jaji alisema mahakama huwa zinatoa maamuzi yake kulingana na ushahidi unaowasilishwa mbele yake.

Alisema waathiriwa wanaweza kuisaidia Idara ya Mahakama kuwanasa wahusika kwa kulinda ushahidi.

“Ninamrai yeyote ambaye amedhulumiwa kimapenzi au kubakwa, kutozingatia miito kwamba wanapaswa kuoga mara moja baada ya visa hivyo. Badala yake, wanapaswa kufika katika hospitali iliyo karibu mara moja ili kuwawezesha wahudumu wa afya kuchukua ushahidi wa kimatibabu. Hilo litaziwezesha idara husika kuwanasa wahusika na kudhihirisha kikamilifu kuwa walishiriki kwenye unyama kama huo,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Wajackoyah kuvumisha biashara ya bangi, nyoka

Wito wafungwa washauriwe kabla kuachiliwa

T L