• Nairobi
  • Last Updated May 22nd, 2024 5:30 PM
Wadudu wa ‘Nairobi fly’ wanavyohangaisha Wakenya msimu wa El Nino na kuwaacha na vidonda vibaya

Wadudu wa ‘Nairobi fly’ wanavyohangaisha Wakenya msimu wa El Nino na kuwaacha na vidonda vibaya

NA WANGU KANURI

HUKU mvua kubwa ya El Nino ikipungua, Wakenya hawajaathirika tu na mafuriko au kukosa makazi bali pia kung’atwa na mdudu aina ya Narrow Bee Fly anayetambuliwa na wengi kama Nairobi Fly.

Maureen Wanjiru, ni mmojawapo wa Wakenya ambao wameng’atwa na mdudu huyu huku madhara yake yakijionyesha uso mzima.
Bi Wanjiru anasimulia kuwa ameng’atwa mara mbili na mdudu huyu, mwaka jana na mwaka huu.

“Mara ya kwanza, nilihisi ni kama uso wangu ulikuwa unawashwa sana. Akilini nikadhani ni uchovu tu kwa hivyo nikaenda kupumzika. Nilipoamka, sikuwa naweza kufungua macho na uso ulikuwa umefura ajabu,” anaeleza.

Matibabu zaidi

Baada ya kuzuru zahanati shuleni, Bi Wanjiru alirudi nyumbani ili kupata matibabu zaidi.

“Wakati huo, uso ulikuwa umefura lakini ulikuwa unachambuka. Nikapewa dawa za kupaka na kumeza na nikarudi shuleni,” anakumbuka.

Kama mara ya kwanza, Bi Wanjiru hakujua mdudu huyo akimng’ata mara ya pili, huku dalili za mtagusano na mdudu huyu zikiwa ishara mwilini mwake.

“Wakati huu zilikuwa zimevamia shule tena kwa wingi. Isitoshe, dalili za kung’atwa na mdudu huyu zilikuwa kali ikilinganishwa na mara ya kwanza. Nilihisi uchungu mwingi sana usoni, nikawashwa, kisha uso ukaanza kuchambuka, na nikapata pele zilizokuwa zinajaa usaha.”

Hata ingawa alizuru zahanati na kupata tembe, Bi Wanjiru bado anauguza athari za kung’atwa na mdudu huyu.

Utamjuaje mdudu huyu?

Dkt Nancy Omwenga, mtalaamu wa ngozi kutoka hospitali ya Mama Lucy Kibaki anasema kuwa anapokuwa mzima, mdudu huyu huwa na urefu wa milimita 7 hadi 10 na upana wa milimita 0.5 hadi 1.

Nairobi Fly huwa na kichwa cheusi, huku sehemu za mwili wake zikiwa na rangi ya nyekundu au majano na sehemu zingine nyeusi.

“Wanapenda kujikunja wanaposumbulia au kukimbia. Wanaweza kuruka lakini wanapendelea kukimbia au kusonga kwa haraka,” anaeleza.

Kwa mujibu wa Dkt Omwenga, mdudu huyu huishi sehemu zilizo na joto na unyevunyevu au wakati wa mvua ndefu. Nairobi Fly ni wanyama wa usiku lakini huvutiwa sana na mwangaza.

Anapokung’ata, mgonjwa hupata dalili za kuwa na upele wa ghafla wa rangi nyekundu ambao unaweza kuwa na vijipu.

“Upele huu huwa na muwasho na maumivu makali. Huwa unaanza kuonekana saa 24 hadi 48 baada ya kugusana na nzi. Upele huu kisha hupona ndani ya wiki moja au siku 10, ukipukutika na kuacha makovu au alama kwenye ngozi,” anasema Dkt Omwenga.

Kujilinda

Ili kuzuia mtagusano na Nairobi Fly, Dkt Omwenga anashauri kuwa ni vyema kufunga milango na dirisha au kutumia vyandarua.
Kuzima taa za haswa zile zinazokuwa karibu na madirisha.

Anaongezea, “Epuka kusimama karibu na taa usiku. Epuka kuwa kwenye mazingira ya mimea mingi iliyo karibu na majengo. Safisha nyumba na mazingira ya nyumbani.

Tumia neti zilizotibiwa na dawa za kuua wadudu na uvae nguo ndefu wakati unaenda katika maeneo yanayovamiwa na mdudu huyu (endemic areas).”

Sikukuu

Iwapo unasafiri nyakati hizi za kusherehekea Sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya katika maeneo haya sugu ya mdudu huyu, ni vyema kubeba krimu ya kuzuia kuguswa naye (insect repellent cream/lotion).

Hali kadhalika, Dkt Omwenga anashauri kuwa iwapo mdudu huyu atakung’ata, unaweza zuia kuwashwa usipomshika au hata kumkanyaga.

“Ikiwa atatua kwenye ngozi, usimuulie hapo badala yake mpulize au umuwekee karatasi atakayotembelea juu kisha umuondoe.”

Isitoshe, Dkt Omwenga anafafanua kuwa eneo hilo lililoguswa na Nairobi Fly, linapaswa kuoshwa kwa maji mengi na sabuni kwa kufinya kwa barafu ili kuzuia mwasho.

“Nguo zilizoguswa na mdudu huyu pia zinapaswa kuoshwa mara moja. Yote tisa kumi, tafuta ushauri wa daktari kwa matibabu.”

Madhara ya muda mrefu

Hata hivyo, Nairobi Fly huweza kusababisha madhara ya muda mrefu ambayo Dkt Omwenga anaeleza ni pamoja na sehemu za ngozi kuwa nyeusi sana kuliko rangi kawaida (hyperpigmentation).

Kwa upande mwingine, ngozi inaweza kuwa na mabaka sababu ya melanini inatengeneza rangi ya ngozi, macho na nywele kuwa kidogo (hypopigmentation).

“Mgonjwa pia anaweza pata makovu kutegemea na ukali wa uvimbe wa mdudu huyo (dermatitis),” anaongezea.

Hata hivyo, Dkt Omwenga anasema kuwa mtu anaweza zuia madhara ya muda mrefu ya Nairobi Fly kwa kuzuru hospitalini mapema ili uvimbe wake uweze kutibiwa haraka.

“Mgonjwa anapopata matibabu yanayofaa, mwili wake utaweza kukabiliana na ukali wa mdudu huyo.”

  • Tags

You can share this post!

El Nino: Mbunge alalamikia ubaguzi katika usambazaji wa...

Mbunge apendekeza CEO wa IEBC apewe mamlaka ya mwenyekiti...

T L