• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 8:50 AM
Bruno Fernandes atia saini mkataba mpya wa mwaka mmoja kambini mwa Man-United

Bruno Fernandes atia saini mkataba mpya wa mwaka mmoja kambini mwa Man-United

Na MASHIRIKA

KIUNGO Bruno Fernandes, 27, ametia saini mkataba mpya wa mwaka mmoja zaidi kambini mwa Manchester United.

Nyota huyo raia wa Ureno alitua ugani Old Trafford mnamo Januari 2020 baada ya kuagana rasmi na Sporting CP kwa kima cha Sh6.6 bilioni. Sasa atakuwa huru kurefusha kandarasi yake kambini mwa Man-United kwa miezi 12 zaidi baada ya ile ya sasa kutamatika mwishoni mwaka wa 2026.

Fernandes amefungia Man-United mabao 49 kutokana na mechi 117 zilizopita katika mashindano yote. “Kuna mengi zaidi ambayo nataka kuyafikia nikichezea Man-United. Hayo ndiyo malengo ambayo pia kila mchezaji na mfanyakazi wa kikosi hiki anayo. Kubwa zaidi ni kwamba tunapania kuwapa mashabiki wetu mafanikio ambayo wanastahili kujivunia,” akasema nyota huyo ambaye amechangia mabao 39 ambayo yamefumwa wavuni na waajiri wake wa sasa.

Ujio wa Fernandes kambini mwa Man-United ulipiga jeki mabingwa hao mara 20 wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na akatawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka wa kikosi hicho licha ya kusajiliwa katikati ya msimu wa 2019-20. Hadi kusajiliwa kwake, hakukuwa na mchezaji yeyote mwingine katika kikosi cha Man-United aliyekuwa amechangia idadi kubwa ya mabao kambini mwa miamba hao.

Isitoshe, Fernandes alitawazwa mfungaji bora wa Man-United kwa mabao 28 kutokana na mechi za msimu mzima wa 2020-21. Hata hivyo, matokeo yake msimu huu wa 2021-22 yamekuwa yakisuasua huku Man-United kwa sasa wakikamata nafasi ya sita kwenye msimamo wa jedwali la EPL. Matokeo duni ya Man-United muhula huu yalichangia kutimuliwa kwa mkufunzi Ole Gunnar Solskjaer na nafasi yake kutwaliwa na kocha mshikilizi Ralf Rangnick.

You can share this post!

Dynamo Kyiv kucheza dhidi ya vikosi vya haiba barani Ulaya...

KPC yadai kuwa mafuta ya kutosha kwenye hifadhi zake huku...

T L