• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
Rennes waangusha miamba PSG katika Ligi Kuu ya Ufaransa

Rennes waangusha miamba PSG katika Ligi Kuu ya Ufaransa

Na MASHIRIKA

MIAMBA Paris Saint-Germain (PSG) walipoteza mchuano wa pili mfululizo ugenini katika Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) baada ya Rennes kuwacharaza 1-0 mnamo Jumapili usiku.

Nahodha Hamari Traore alifungia Rennes bao la pekee na la ushindi katika mchuano huo baada ya kushirikiana vilivyo na Adrien Truffert.

Kylian Mbappe aliyetokea benchi katika kipindi cha pili alipoteza nafasi ya wazi ya kusawazishia PSG baada ya kupaisha kombora lake licha ya kusalia peke yake na kipa wa Rennes.

Licha ya kichapo, PSG walisalia kileleni mwa jedwali la Ligue 1 kwa alama 47 japo ni pengo la alama tatu pekee ndilo linawatenganisha na Lens wanaokamata nafasi ya pili baada ya kupepeta Auxerre 1-0, Jumamosi.

Chini ya kocha Christophe Galtier, PSG walifungua mwaka huu wa 2023 kwa kichapo cha 3-1 ugenini. Walikosa kuelekeza kombora lolote langoni mwa Rennes hadi dakika ya 81 kupitia kwa Juan Bernat aliyeshuhudia fataki yake ikipanguliwa na kipa mzoefu Steve Mandanda.

PSG walitumia mechi dhidi ya Rennes kuwa jukwaa la kumwajibisha chipukizi Warren Zaire-Emery aliyeweka rekodi ya kuwa mchezaji mchanga zaidi kuwahi kunogesha pambano la Ligue 1 akiwa na umri wa miaka 16 na siku 313.

Kwingineko, Wissam Ben Yedder alifunga mabao matatu katika kipindi cha dakika 14 na kusaidia AS Monaco kuponda Ajaccio 7-1.

Axel Disasi, Krepin Diatta na Breel Embolo (mawili) walifunga mabao mengine ya Monaco waliopaa hadi nafasi ya nne jedwalini kwa alama 37 sawa na Rennes.

MATOKEO YA LIGUE 1 (Jumapili):

Rennes 1-0 PSG

Lille 5-1 Troyes

Angers 1-2 Clermont

Montepellier 0-3 Nantes

Reims 0-0 Nice

Toulouse 1-1 Brest

Monaco 7-1 Ajaccio

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

MAPISHI KIWETU: Firigisi ya kuku

Chelsea waangusha Palace ugani Stamford Bridge na...

T L