• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 6:50 AM
Maswali yazuka kuhusu aliko ‘Sultani’ Joho

Maswali yazuka kuhusu aliko ‘Sultani’ Joho

NA WINNIE ATIENO

TANGU alipomkabidhi mamlaka Gavana wa Mombasa Abdulswamad Nassir mnamo Septemba 23, aliyekuwa gavana wa kaunti ya Mombasa Bw Ali Joho, hajaonekana hadharani.

Kukosekana kwake kwa machoni pa umma kumeibua minong’ono, huku waliokuwa wakitumia jina lake kuendesha biashara jijini Mombasa wakiachwa kwenye mataa.

Licha ya hayo, Bw Joho amekuwa akipakia mitandaoni picha zake akiwa jijini Dubai na taifa la Uholanzi.

Gavana huyo ambaye kwa kawaida hupenda kuonyesha wafuasi wake katika mitandao ya kijamii, anavyofurahia maisha ya kifahari ameendelea kufanya hivyo.

Amekuwa akiendelea kutupia video hizo akiwapiga vijembe adui zake kwa wafuasi wake 1.2m kwenye mitandao ya Instagram, Facebook na 326,000 katika mtandao wa TikTok.

Aliyekuwa mkuu wa wafanyakazi katika serikali yake Bw Joab Tumbo, anaelezea kuwa bosi wake huyo si yule wa kitambo.

Kwa sasa anafuatilia mambo yake ya kibinafsi.

“Atarejea Kenya hivi karibuni. Kuna maisha baada ya siasa,” alisema Bw Tumbo.

Bw Joho alisafiri kisirisiri kuelekea mataifa ya nje ya nchi, pindi tu baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Miezi kadhaa baadaye palitokea fununu kuwa alikuwa amegura chama cha ODM na kuunda chama chake binafsi.

Licha ya hayo, kinara wa chama cha ODM alipuuzilia mbali tuhuma hizo akieleza kuwa Joho alikuwa sehemu kuu ya chama cha ODM.

“Yupo nje ya nchi kwa sasa ila atarudi. Sisi huongea kila wakati hata wiki hii tumezungumza. Akirudi ataungana na chama chetu na kutoa mchango wake. ODM iko imara na haivunjiki. Ni kama tu Azimio ambayo iko imara,” alisema Bw Odinga wiki mbili zilizopita, katika kanisa la Anglikana jijini Mombasa.

Kigogo huyo ambaye alijulikana kuwa kigogo wa siasa eneo la Pwani, aliachwa njia panda baada ya Bw Odinga kupoteza katika uchaguzi mkuu.

Aidha alikuwa ateuliwe kuwa Waziri wa Ardhi katika serikali ya Bw Odinga iwapo angeshinda.

Alikuwa ameahidi kuwa, angesuluhisha matatizo yote ya ardhi, kabla ya dau la Azimio kuzama.

Bw Odinga pia alipinga madai ya kuwa alikuwa amepoteza ufuasi katika eneo la Pwani kwa rais Ruto, na kuwa kukosekana kwa Bw Joho Mombasa kulikuwa kumeathiri kambi yake.

Eneo hilo limekuwa uwanja huru baada ya wanasiasa wa Kenya Kwanza kutumia nafasi ya kuwa Bw Joho hayupo, kuingia na kusuka mikakati ya kisiasa.

Bw Joho na Spika wa Seneti Bw Amason Kingi ndio walikuwa wakiisaidia ODM kung’aa katika eneo hilo.

Baada ya Kingi kujiunga na serikali ya Dkt William Ruto, kutokuwepo kwa Bw Joho, kumeacha eneo hilo likiyumbayumba kisiasa.

Bw Joho alionekana mara ya mwisho akila chamcha na mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki Bw Suleiman Shahbal na msanii wa Tanzania Ommy Dimpoz pamoja na marafiki wengine Dubai.

Saa aliyokuwa amevaa iliibua gumzo mitandaoni, baada ya kugunduliwa kuwa saa hiyo aina ya Richard Mille (RM11-01) ni yenye thamani ya takriban Sh50 milioni.

  • Tags

You can share this post!

Beki wa Kibera Black Stars FC asema klabu imejiwekea...

Ruto akana kumwekea mtego Gachagua

T L